Mkazi wa Mtaa wa Mateka, Manispaa ya Songea, Denis Komba
(26) afariki dunia baada ya nyoka wake aliyekuwa amembeba kwenye mfuko wa
jaketi kuuawa na wananchi.
Komba alifariki dunia katika hospitali ya Rufaa Songea mkoa
wa Ruvuma (Homso) ambako alilazwa baada ya watu wenye hasira kumuua kwa mawe na
fimbo nyoka wake huyo.
Mashuhuda wanaeleza kuwa kabla ya wananchi kumuua nyoka huyo,
Komba aliwasihi wasifanye hivyo kwa kuwa wakimuua na yeye angekufa, lakini ombi
lake hilo halikusikilizwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, siku ya tukio Komba
alikodi pikipiki ya Kassian Haule (24) ambaye ni mkazi wa Mpitimbi, yenye namba
za usajili MC 724 AKB ili apelekwe nyumbani kwake mtaa wa Mateka.
Akisimulia tukio hilo, alisema alipofika katika eneo la
Benki ya Posta ya zamani barabara kuu ya Sokoine, dereva wa pikipiki alihisi
kuna kitu kinamtekenya na kumgonga gonga kwa nyuma, ndipo alipogeuka nyuma na
kumwona abiria wake amebeba nyoka mkubwa huku amesimamisha kichwa.
Haule alisema, baada ya kumuona nyoka huyo aliruka kutoka
kwenye pikipiki na kuanguka pembeni mwa barabara na abiria wake alimwachia yule
nyoka ambaye alikimbilia kwenye kalavati la maji.
Aliongeza kuwa ndipo alipopiga kelele za kuomba msaada na
kundi la vijana waendesha pikipiki wenzake walifika eneo hilo la tukio kwa
lengo la kumsaidia mwenzao juu ya maswahiba yaliyompata hadi kumfanya apige
kelele.
Alisema kabla ya vijana hao hawajafanya jambo lolote, Komba
aliwaomba vijana hao na watu wengine waliofika katika eneo hilo wasimpige nyoka
wake kwani iwapo watampiga na kufa yeye pia atapoteza maisha. Kutokana na
maneno hayo, Haule alimtoa nyoka huyo ndani ya kalavati na kwa kushirikiana na
vijana wenzake walianza kumpiga nyoka huyo hadi kufa.
Alisema wakati wanampiga nyoka huyo, Komba ambaye ndiye
mmiliki wa nyoka huyo naye alianza kulegea kisha akaanguka chini huku akitokwa
na mapovu mdomoni na puani.
Habari zinasema kuwa,baada ya Komba kuanguka alikimbizwa
hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu; hata hivyo juhudi za madaktari na
wauguzi wa hospitali za kuokoa maisha yake zilishindikana kwani Komba
alifariki.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji,
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa mwili wa marehemu haukuwa
na jeraha lolote na umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika
hospitali ya rufaa Songea.
Alisema nyoka aliyeuawa na wananchi amechukuliwa na idara ya
maliasili na uchunguzi zaidi ya tukio hilo unaendelea ili kubaini kiini cha
tukio hilo la kuuawa kwa nyoka na kisha mmiliki wake naye kufa. Kamanda
Mwombeji alisema, kwa upande wa dereva wa pikipiki yeye anaendelea vizuri na
anapatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Ruvuma.
Aidha Kamanda Mwombeji, ametoa rai kwa wananchi kuacha mara
moja kumiliki nyara za serikali zinazoweza kuwaletea madhara kama vile majeraha
au vifo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni