SERIKALI imezindua Mpango Kazi wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto
unaolenga kushirikisha wadau wengine katika jitihada jumuishi za kuzuia ukatili
dhidi ya wanawake na watoto na hivyo kusaidia wahanga wa ukatili huo kupata
huduma stahiki ili kudhibiti ukatili nchini.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi huo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Ummy Mwalimu kwa niaba ya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema
jamii inajukumu la kuhakikisha ukatili wa wanawake na watoto unapigwa vita kwa
vitendo.
“Serikali
inaikumbusha jamii kupambana na vitendo vya ukatili kwani ukatili unafanyika
kuanzia ngazi ya familia hivyo ni jukumu la wananchi kutoa taarifa za ukatili
wa wanawake na watoto ili vyombo vya dola viweze kuwachukulia hatua za
kisheria”, alisema Waziri Ummy.
Pia Waziri Ummy ameongeza kuwa Kumekuwepo na
matukio mengi ya ukatili yanayosababishwa na mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja
na umaskini katika familia, mila na desturi potofu zenye athari katika jamii,
malezi na makuzi mabovu na sheria kandamizi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa
Asasi za Kiraia zinazoshughulika na utetezi wa haki za watoto (TCRF) Bw. Erick Guga
amesema watoto ndiyo wahanga wakubwa wa ukatili huu hivyo ni wakati muafaka kwa
mpango kazi kuanza kazi ili kuwanusuru wanawake na watoto katika ukatili.
“Mpango Kazi huu wa Kutokomeza
Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto nchini Tanzania utakuwa ndiyo dira kwa
wadau wote wa masuala ya maendeleo ya wanawake na watoto hapa nchini hivyo ni
vema Serikali kushirikiana na wadau kila inapohitajika”, alisema Bw. Guga.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Sihaba Nkinga amesema kuwa, kabla
ya kuandaliwa kwa Mpango Kazi huu, Tanzania ilikuwa na mipango kazi minane (8)
ya kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Aidha Bi. Sihaba ameongiza kuwa
mipango hiyo haikuwa na mfumo wa pamoja wa kufuatilia na kutathmini ufanisi
unaopatikana, Vilevile, kutokana na madhara ya ukatili dhidi ya wanawake na
watoto katika maendeleo ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, wakuu wa nchi
wanachama waliazimia kwa pamoja kutokomeza ukatili huo kupitia utekelezaji wa
lengo Na. 5 na 6 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo 2030.
“ Tanzania ni kati ya nchi nne (4)
za kwanza duniani na nchi pekee katika Afrika iliyowezeshwa kupitia jukumu
lilioanzishwa la kusaidia nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuandaa mpango wa
kuzuia na kuitikia afua za kudhibiti ukatili ili kuwa na mipango thabiti ya
upatikanaji wa haki, usawa na maendeleo kwa wote”, alisema Bibi.Sihaba.
Akieleza katika uzinduzi huo
Mkurugenzi Sera na Mipango Emmanuela Achayo aliseama kuwa Mpango kazi huo wa
aina yake una maeneo makuu manane (8) yatakayotekelezwa na wadau wa maendeleo
ya wanawake na watoto.
“Maeneo hayo ni kuimarisha uchumi
wa kaya, Uzuiaji wa mila na desturi zenye madhara na Uboreshaji wa mazingira
salama katika jamii”, alisema Achayo.
Maeneo mengine ni Kuendeleza mazingira
salama ya mafunzo shuleni na stadi za maisha na kuhuisha mahusiano, malezi na
makuzi katika familia, Utekelezaji na usimamizi wa sheria, Utoaji huduma kwa
wahanga na Uratibu, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mpango kazi wa
miaka mitano kuanzia mwaka 2017/2018 hadi 20121/21022.
Mpango huu mahususi unatarajiwa
kuwa na matokeo makubwa baada ya miaka mitano ya utekelezaji kwani utawezesha
kuondoa ukatili dhidi ya wanawake kwa asilimia 50 kufikia mwaka 2021/2022; na
Kuondoa ukatili dhidi ya watoto kwa asilimia 50 kufikia mwaka 2021/2022,
na hivyo kuleta mabadiliko makubwa kwa kuwa na familia salama, na jamii yenye
utulivu.
Kazi zitakazotekelezwa na kila
mdau kuanzia familia, jamii, halmashauri, mikoa, wizara, sekta binafsi, asasi
za Kiraia na wabia wa maendeleo Mpango umeweka mfumo fungamanishi wa uratibu,
ufuatiliaji na tathmini ambao utaratibiwa katika ngazi ya Taifa na Ofisi ya
Waziri Mkuu, ngazi ya mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa, na ngazi ya
halmashauri na Wakurugenzi Watendaji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni