Rais John Magufuli akiwapungia
wananchi waliofurika kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam wakati
alipoingia kwenye uwanja huo kuongoza sherehe za miaka 55 ya Uhuru
Desemba 9, 2016.
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu akikagua gwaride kwenye sherehe za miaka 55 ya uhuru.
Rais John Magufuli akisalimiana
na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Uhuru jijini
Dar es salaam kuongoza sherehe za miaka 55 ya Uhuru jijini Dar es salaam
Desemba 9, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Rais wa
Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein katika sherehe za miaka 55 ya uhuru kwenye
uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam Desemba 9, 2016.
HABARI.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Magufuli amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza jitihada
zilizoachwa na Serikali za awamu zilizopita ili kuzidi kuwaletea
maendeleo Watanzania.
Ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa
maadhimisho ya sherehe za miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania bara yaliyofanyika
katika uwanja wa uhuru Jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
imeanza jitihada za kuboresha huduma za maendeleo ya jamii, ambapo katika
bajeti ya mwaka 2016/17 imeamua kutenga asilimia 40 ya bajeti katika
miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo umeme, miundombinu, afya, elimu.
“Mbali na kujiwekea vipaumbele mbalimbali kwa
maendeleo ya nchi, kumekuwa na changamoto kadha wa kadha zinazozikabili nchi
ikiwemo ufisadi, rushwa ndani ya baadhi ya watendaji” alisema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli alisema juhudi zinazoendelea
kufanywa na Serikali ni kuboresha maslahi kwa watanzania kwa kuchukua hatua
mbalimbali za kuwawajibisha wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na
ufisadi.
Akifafanua zaidi Rais Magufuli aliwataka watanzania
kudumisha amani na kulinda muungano uliyopo kwani amani ni msingi wa maendeleo
ya nchi bila amani hakuna maendeleo.
Rais Magufuli pia alitoa wito kwa watanzania
kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwani kila mwananchi ana haki ya kufanya
kazi, na kusema kuwa waasisi wa nchi walileta uhuru kwa maendeleo ya nchi kwani
Uhuru ni kazi.
“Serikali ya Tanzania imejipanga kufanya kazi,
tutafanya kazi kwelikweli, watendaji niliowachagua wanafanya kazi hivyo
watanzania kwa ujumla mnatakiwa kuonesha ushirikiano kwao kwa maendeleo ya nchi
yetu” alisema Rais Magufuli.
Mbali na hayo Rais Magufuli alisema kuwa ndani ya
miaka 55 ya Uhuru Tanzania imepata mafanikio makubwa ambapo Tanzania imelinda
Uhuru wa nchi, sambamba na kulinda mipaka iliyopo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni