Alhamisi, 29 Desemba 2016

AMUUA RAFIKI YAKE NA KULA UBONGO WAKE NA SEHEMU ZA SIRI .

JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya, linamshikilia mchimba dhahabu, Shija Salum (38), mkazi wa Kahama mkoani Shinyanga kwa tuhuma za kumuua rafiki yake na kula ubongo wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba pamoja na mtuhumiwa huyo kula ubongo wa rafiki yake huyo aliyetambuliwa kwa jina moja la Shija, pia alitafuna sehemu zake za siri baada ya kuzikata.

Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, tukio hilo lilitokea Desemba 25, mwaka huu, usiku katika Kijiji cha Manyanya, Kata ya Makongorosi, Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.

Alisema mtuhumiwa na marehemu walifika kijijini hapo wakitokea Shinyanga miezi mitatu iliyopita.

“Inasemekana wawili hao walikuwa ni marafiki kwani walifika wilayani Chunya, Kata ya Makongolosi kwenye machimbo ya dhahabu yanayomilikiwa na mfanyabiashara mmoja aitwaye Teddy Mwantega.

“Siku hiyo ya tukio, marehemu Shija, alikuwa amejilaza mahali na hapo ndipo alipofika rafiki yake huyo, akiwa na panga mkononi na kumkata kwa nguvu kichwani.

“Baada ya hapo, alimvua nguo na kuzikata sehemu zake za siri na kuzishika mkononi.

“Wakati akiwa na sehemu hizo za siri mkononi, alichukua ubongo wa marehemu na kuula, kisha akatafuna zile sehemu za siri.

“Kwahiyo, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika,” alisema Kamanda Kidavashari.

Jumatano, 28 Desemba 2016

PROF. MBARAWA AKUMBUSHA KAMPUNI ZA MAWASILIANO KUJISAJILI SOKO LA HISA.



WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amezitaka Kampuni za Mawasiliano kukamilisha taratibu za usajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam kwa kuuza asilimia 25 ya hisa zote kadri ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana inavyoelekeza mwishoni mwa mwaka huu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Prof. Mbarawa ametaja kampuni hizo kuwa ni zile zenye leseni za mawasiliano zilizotolewa kabla ya tarehe 1 Julai 2016 kwa ajili ya Miundombinu ya Mawasiliano, Huduma za Mawasiliano, na Huduma za Matumizi.

“Watoa huduma wote wa Mawasiliano wajisajili na kuuza hisa zao kwa wananchi ndani ya mwezi wa Disemba”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa kwa Kampuni zilizopata leseni baada ya tarehe mosi Julai, 2016 watatakiwa kutimiza sharti hilo la kisheria kwa kipindi kisichozidi miaka miwili tangu kusajiliwa.

Waziri Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa Kampuni zitakazokiuka Sheria hiyo zitachukuliwa hatua za kisheria kupitia kifungu cha 21 (C) cha EPOCA, 2010.
Aidha, amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kununua hisa hizo na kuwa sehemu ya wamiliki wa makampuni ya Mawasiliano ili kuongeza kipato na kushiriki katika maamuzi ya kampuni hizo.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

HII NI AJABU YA KUFUNGA MWAKA 2016 ILIOTOKEA MKOANI SONGEA.



Mkazi wa Mtaa wa Mateka, Manispaa ya Songea, Denis Komba (26) afariki dunia baada ya nyoka wake aliyekuwa amembeba kwenye mfuko wa jaketi kuuawa na wananchi.

Komba alifariki dunia katika hospitali ya Rufaa Songea mkoa wa Ruvuma (Homso) ambako alilazwa baada ya watu wenye hasira kumuua kwa mawe na fimbo nyoka wake huyo.

Mashuhuda wanaeleza kuwa kabla ya wananchi kumuua nyoka huyo, Komba aliwasihi wasifanye hivyo kwa kuwa wakimuua na yeye angekufa, lakini ombi lake hilo halikusikilizwa.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, siku ya tukio Komba alikodi pikipiki ya Kassian Haule (24) ambaye ni mkazi wa Mpitimbi, yenye namba za usajili MC 724 AKB ili apelekwe nyumbani kwake mtaa wa Mateka.

Akisimulia tukio hilo, alisema alipofika katika eneo la Benki ya Posta ya zamani barabara kuu ya Sokoine, dereva wa pikipiki alihisi kuna kitu kinamtekenya na kumgonga gonga kwa nyuma, ndipo alipogeuka nyuma na kumwona abiria wake amebeba nyoka mkubwa huku amesimamisha kichwa.

Haule alisema, baada ya kumuona nyoka huyo aliruka kutoka kwenye pikipiki na kuanguka pembeni mwa barabara na abiria wake alimwachia yule nyoka ambaye alikimbilia kwenye kalavati la maji.

Aliongeza kuwa ndipo alipopiga kelele za kuomba msaada na kundi la vijana waendesha pikipiki wenzake walifika eneo hilo la tukio kwa lengo la kumsaidia mwenzao juu ya maswahiba yaliyompata hadi kumfanya apige kelele.

Alisema kabla ya vijana hao hawajafanya jambo lolote, Komba aliwaomba vijana hao na watu wengine waliofika katika eneo hilo wasimpige nyoka wake kwani iwapo watampiga na kufa yeye pia atapoteza maisha. Kutokana na maneno hayo, Haule alimtoa nyoka huyo ndani ya kalavati na kwa kushirikiana na vijana wenzake walianza kumpiga nyoka huyo hadi kufa.

Alisema wakati wanampiga nyoka huyo, Komba ambaye ndiye mmiliki wa nyoka huyo naye alianza kulegea kisha akaanguka chini huku akitokwa na mapovu mdomoni na puani.

Habari zinasema kuwa,baada ya Komba kuanguka alikimbizwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu; hata hivyo juhudi za madaktari na wauguzi wa hospitali za kuokoa maisha yake zilishindikana kwani Komba alifariki.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa mwili wa marehemu haukuwa na jeraha lolote na umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya rufaa Songea.

Alisema nyoka aliyeuawa na wananchi amechukuliwa na idara ya maliasili na uchunguzi zaidi ya tukio hilo unaendelea ili kubaini kiini cha tukio hilo la kuuawa kwa nyoka na kisha mmiliki wake naye kufa. Kamanda Mwombeji alisema, kwa upande wa dereva wa pikipiki yeye anaendelea vizuri na anapatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Ruvuma.

Aidha Kamanda Mwombeji, ametoa rai kwa wananchi kuacha mara moja kumiliki nyara za serikali zinazoweza kuwaletea madhara kama vile majeraha au vifo.



Jumanne, 27 Desemba 2016

MKUU WA MKOA WA SINGIDA AJITOSA KUTEKELEZA AGIZO LA RAIS MAGUFURI.



Serikali mkoani Singida, inatarajia kujenga kiwanja kikubwa cha ndege kitakachowezesha ndege kubwa za abiria na mizigo kutua, ikiwa ni maandalizi ya kunufaika na fursa lukuki za kiuchumi na kijamii zitakazopatikana,baada ya makao makuu ya nchi kuhamia jirani Dodoma.

Hayo yamesemwa na mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Rehema Nchimbi wakati akizungumza kwa mara ya kwanza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Alisema wakati wo wote kuanzia sasa kazi ya kutafuta eneo la kujenga kiwanja hicho na taratibu zingine muhimu, zitaanza,na amewataka wananchi wawe tayari kutoa ushirikiano.

“Msukumo wa ujenzi wa kiwanja kikubwa cha ndege,umekuja baada ya rais Dk.Magufuli kuutaka uongozi wa mkoa kuangalia uwezekano wa kujenga kiwanja hicho. Ushauri au mapendekezo yanayotolewa na mkuu wananchi, hayo ni maagizo rasmi, kwa hiyo sisi tulio chini yake, tutajitahidi uwanja huo unajengwa haraka,” alisema na kuongeza.

“Maadamu Rais ameona umuhimu wa uwanja huo na yeye katika serikali yake,anao uwezo mzuri wa fedha,sisi wakazi wa mkoa wa Singida tunachopaswa kufanya,ni kuchangamkia haraka uwanja unapatikana na ujenzi unaanza.”

Akifafanua, alisema serikali ya awamu ya tano imelenga nchi kuwa kwenye uchumi wa kati, hivyo kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi inayochochea ukuaji wa uchumi, huwa haina kigugumizi katika kutoa fedha.

Akiijengea nguvu hoja yake hiyo, mkuu huyo wa mkoa, alisema hatapenda kuona aina yo yote ya urasimu wa kuchelewesha ujenzi wa uwanja mkubwa wa ndege.

Kwa upande wa wananchi, amewataka watoe ushirikiano wa hali ya juu katika upatikanaji wa uwanja na ushirikiano huo usiishie hapo, uendelee hadi hapo kiwanja kitakapomalizika kujengwa.

“Mimi nitumie fursa hii kuwasihi wananchi katika hili la ujenzi wa uwanja wa ndege mkubwa, walipe kipaumbele cha kwanza na fidia wawe na subira. Waamini tu kwamba ni lazima watafidiwa. Nina uhakika kiwanja kitakapoanza kufanya kazi, wananchi watanufaika kiuchumi kwa kiwango kikubwa, na pengine watatanza kusema kiwanja hicho kimechelewa kujengwa,” alisema Dk. Nchimbi.

Katika hatua nyingi, alisema Serikali yake itafanya juhudi za kuhakikisha mkoa wa Singida, una kuwa wa viwanda vikubwa, ili kutoa nafasi makao makuu ya nchi Dodoma, kupumua na kujikita zaidi kwenye shughuli ya kuiongoza nchi.

“Pia nitahakikisha mkoa wangu unakuwa na uwezo wa kujilisha na kulisha makao makuu ya nchi. Tuna kila sababu ya kulifikia lengo hilo. Tutahimiza kilimo cha umwagiliaji na kuchimba mabwawa makubwa kwa ajili ya kilimo cha malisho ya mifugo,” alisema.

Jumanne, 20 Desemba 2016

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI ASIKITISHWA NA VITENDO VYA MAUAJI YA WAKULIMA NA WAFUGAJI MKOANI PWANI



Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mwigulu Nchemba akiwa na  Mbunge wa Jimbo la Kibaha  mjini Silvestry Koka  wakiangalia gari ambayo ilikamatwa Wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani ikiwa na wahamiaji haramu wapatao  150 ambao ni  raia  kutoka nchini Ethiopia ambao walikamatwa wakati wakiwa  wapo safari kuelekea mikoa ya kusini.

HABARI.
ONGEZEKO la wimbi la migogoro ya ardhi kila kukicha katika baadhi ya maeneo katika  Mkoa wa  Pwani  kati ya jamii ya wakulima na wafugaji na kupelekea wakati mwingine kuibuka kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe   ambayo yanasababisha hali ya uvunjifu wa amani na  baadhi ya viongozi na wananchi  wengine  kupoteza maisha  kikatili kimeundwa kikosi kazi maalumu kwa ajili ya kuweza  kukomesha kabisa vitendo hivyo.

Matukio ya namna hiyo   katika Mkoa wa Pwani yanaonekana  kumsikitisha na kumlazimu Waziri wa mambo ya ndani Mwigulu Nchemba kuingilia kati sakata hilo kwa kutangaza rasmi kupambana vilivyo na watu wote ambao watabainika wanajihusisha na vitendo hivyo vya mauaji ili waweze kukamatwa haraka  na kuweza kufikishwa katika vyombo vya dola ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia  kama hiyo.

Waziri nchemba ametoa  agizo hilo wakati wa ziara yake ya kuwatembelea askari polisi, magereza, uhamiaji pamoja zimamoto wa Mkoani Pwani kwa ajili ya kuweza kukagua shuguli mbali mbali  za utekelezaji ya majukumu yao ya kila siku ikiwemo na  kuweza kubaini changamoto   zinazowakabili pamoja na kuweka mikakati  kwa ajili ya kuweza kuzitafutia ufumbuzi.

“Kumekuwepo katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani kuna baadhi ya viongozi wa vijiji pamoja na wakulima na wafugaji kupoteza maisha, kwa hili sisi kama Wizara hatuwezi kulivumilia hata kidogo kwani kwa sasa tumejipanga ii kuweza kuwabaini watu ambao wanahusika katika vitendo hivyo,”alisema Waziri.

Alisema kuwa  anasikitishwa kuona mauaji yanafanyika kitu ambacho ni kinyume kabisa na sheria na taratibu za nchi, kwa mwananchi yoyote kuamua kujichukulia sheria mikononi kwa kufanya vitendo vya mauaji hivyo ameahidi kulivalia njuga suala hilo na wale wote watakaobainika wataweza kuchukuiwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Aidha Waziri Nchemba alibainisha kuwa kutokana na kuwepo  kwa wahamiaji haramu ambao wanaingia nchini bila ya kuwa na vibali Wizara yake imeweka mikakati kabambe ya kuongeza doria usiku na mchana  katika sehemu mbali mbali ikiwemo  mipaka, fukwe za bahari pamoja na bandari bubu amabzo zimekuwa zikitumika kuwapitisha raia hao wa kigeni.

“Tatizo lawahamiaji haramu katika Mkoa wa Pwani bado ni tatizo kubwa kwani imekuwa ndio kama lango la kuingilia pindi wanapokuja  hasa katika maeneo ya Wilaya ya Bagamoyo pamoja na Wilaya ya Kibaha, hivyo sisi katika hili tumeshajipanga ili kuweza kuthibiti njia zote ambazo wamekuwa wakizitumia katika kupita,”alisema Nchemba.

Pia katika hatua nyingine Nchemba alitoa wito kwa wananchi wote kushirikiana bega kwa began a serikali pamoja na vyombo vya dola katika kuwabaini  na kuwafichua watu ambao wanakuwa na mashaka nao kwani wengine wanaingia nchini kwa ajili ya kufanya matukio mbali mbali ya uharifu wa kutumia silaha.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ameiomba serikali ya awamu ya tano kupitia .

Wizara ya mambo ya ndani  kuhakikisha inaongeza vitendea kazi pamoja na kuongeza ujenzi wa vituo vingine vidogo  vya polisi ambavyo vitaweza kusaidia  kuimarisha hali ya ulinzi na usalama pamoja na kupamba na waharifu ambao wanaingia Mkoa wa Pwani kinyemela na kujificha.

Pia Koka alimwomba waziri wa mambo ya ndani kuweka utaratibu wa kuhakikisha vituo vidogo vya polisi vilivyojengwa vinakuwa wazi wakati wote lengo ikiwa ni kuweza kupambana na matukio mbali mbali ya uharifu ambayo yanakuwa yanajitokeza bila ya kuwa na  muda maalumu hivyo vituo vikiwa wazi kutaweza kusaidia kupunguza hali ya uharifu.

MATUKIO ya vitendo vya  mauaji katika baadhi ya maeneo Mkoani Pwani  ambayo yanawahusisha wakulima na wafugaji pamoja na baadhi ya viongozi wengine  bado yanaonekana kuwa ni tishio na kuendelea kufanyika hivyo kunahitajika jitihada za makusudi  zifanyike kutoka serikalini ili kuweza kutatua migogoro hiyo na kurudisha hali ya amani na utulivu  kwa wananchi.