*** Hizi ni Salaam za Kiongozi wa ACT Wazalendo Kwa Wafanyakazi wa Tanzania, Mei Mosi 2017
Ndugu Wafanyakazi
Leo
(JANA )ni siku yenu katika mwaka. Kama ilivyo kawaida siku hii
husherehekewa kwa maadhimisho makubwa ambapo Waajiri (Serikali na Sekta
Binafsi) na waajiriwa hutoa hotuba mbalimbali. Wakati mwengine ni siku
kama siku nyengine tu za miaka ya nyuma, hotuba, ahadi, kula na kunywa.
Hata hivyo Wafanyakazi wa Tanzania wana changamoto nyingi sana na ni
vema kutumia siku hii kutafakari Kwa kina changamoto hizi na kutafuta
majawabu yake.
Sisi
ACT Wazalendo tunaamini katika siasa za Kijamaa, siasa zenye kupigania
zaidi maslahi ya wanyonge, Wafanyakazi, Wakulima, Wavuvi na Wakwezi.
Katika salaam zangu mwaka huu nawaomba mtafakari hotuba yangu hii
niliyotoa Arusha tarehe Machi 25, 2017 na mapendekezo machache
ninayoyatoa mwishoni mwa waraka wangu huu kwenu.
Nchini
Tanzania Wafanyakazi kwenye sekta rasmi ni milioni 2.1 sawa na 9% tu ya
nguvu kazi yote ya Taifa. Hawa wameajiriwa kwenye sekta binafsi (1.4m
sawa na 67%) na sekta ya umma (700,000 sawa na 33%). Hawa wanalipwa
mishahara na posho mbalimbali kama chanzo cha mapato yao.
91%
ya Watanzania wapo kwenye sekta isiyo rasmi na rekodi ya mapato yao
yaweza kuwa kizungumkuti kuipata. Hata hivyo tunajua kuwa wengi
wameajiajiri wenyewe kwenye kilimo na biashara ndogo ndogo, uvuvi,
ufugaji, uchimbaji wa madini na utoaji huduma.
Ni
muhimu kusisitiza kuwa Watanzania wengi hawamo kwenye ajira rasmi au
isiyo rasmi. Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2015 inaonyesha
kuwa Jijini Dar es Salaam kwa mfano ni asilimia 60 tu ya wakazi wake
wapo kwenye ama ajira rasmi au ajira isiyo rasmi na asilimia 40 hawana
kazi yeyote.
Uchambuzi
pekee ambao tunaweza kuufanya kwa sasa ni kwa kutumia vyanzo vya mapato
ya serikali ambapo tutaona mchango wa Wafanyakazi kwenye mapato ya
Serikali kulingana na vyanzo yake vya mapato.
Kwa
mfano, Kitabu cha Mapato ya Serikali Kuu cha mwaka 2016/17 kinaonyesha
kuwa Wafanyakazi wote wa sekta ya Umma na Sekta Binafsi watachangia
jumla ya shilingi trilioni 3 kwenye mapato yote ya Serikali kulinganisha
na wenye mitaji (waajiri) ambao watachangia jumla ya shilingi bilioni
900 tu kutoka kwenye kodi za faida/gawio, ongezeko la mitaji na riba
(taxes on income/interests, profits and capital gains).
Hata
ukitazama miaka miwili ya nyuma utaona kwamba mwaka 2015/16 makampuni
yalichangia shilingi 773 bilioni wakati Wafanyakazi walichangia shilingi
2.2 trilioni na mwaka 2014/15 makampuni yalichangia shilingi 600
bilioni na wafanyakazi shilingi 1.9 trilioni kama kodi zao kwenye mapato
ya Serikali. Kwa kutumia kigezo cha Kodi za Mapato, matajiri (waajiri)
wanachangia robo tu ya mapato yote ya serikali na wafanyakazi
wanachangia robo tatu iliyobakia. Hii inachangia sana kuwepo kwa tofauti
ya kipato ndani ya jamii.
Kwanini
wafanyakazi wanachangia zaidi kuliko wenye mitaji ni swali ambalo
tutalieleza. Sababu kubwa ni kuwa wenye Miraji/Mabepari wana fursa ya
kukwepa kodi kisheria wakati wafanyakazi hawana uwezo huo. Kodi za
wafanyakazi hukatwa moja kwa moja na waajiri kutoka kwenye mishahara
yao.
Kwanini Kodi za Makampuni ni kidogo kuliko za Wafanyakazi?
Wafanyakazi
wao hukatwa kodi zao kutoka kwenye mishahara yao moja kwa moja ikiwemo
pia makato mengine kama michango kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii na
Bima ya Afya. Makato hayo huanzia asilimia 9 kwa mishahara ya ngazi ya
chini mpaka asilimia 30 kwa wenye kulipwa mishahara ya juu kabisa. Kwa
hiyo kodi ya wafanyakazi ni kodi ambayo serikali ina uhakika nayo moja
kwa moja. Kwa takwimu ambazo tumeziona tayari, ni wafanyakazi wa sekta
rasmi tu ndio hubeba mzigo wote wa kodi za wafanyakazi hapa nchini.
Lakini kwanini kodi zinazotokana na mapato ya makampuni ziwe kidogo
kuliko kodi zinazotokana na mapato ya wafanyakazi?
Kwenye
makampuni, Kodi ya Mapato ni asilimia 30 ya faida ambayo kampuni
imepata. Lakini mapato yanayokusanywa kwenye kodi hii ni kidogo sana
kama tulivyoona, shilingi bilioni 900 tu kati ya mapato yote ya serikali
mwaka 2016/17 sawa na asilimia nne tu ya mapato yote ya serikali
yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania. Hali halisi hii sio ya
Tanzania peke yake.
Mwanazuoni
Thomas Piketty anaeleza kuwa "Ingawa kodi za faida za makampuni ni kati
ya asilimia 40 - 50 kwenye nchi za magharibi, mapato kwenye kodi hizi
hayazidi asilimia 2.5 - 3 ya Pato la Taifa. Nadharia ya faida inayotozwa
kodi ni nyembamba kuliko nadharia ya mapato ghafi ya ziada kwa sababu
makampuni huondoa gharama za uchakavu wa mitambo, riba kwa mikopo na
hata gharama za bima. Kodi kwenye faida imegubikwa na matundu mengi
kwenye mfumo mzima wa kodi duniani" (msisitizo ni wangu).
Matundu
haya ndiyo njia za ukwepaji kodi zinazofanywa na makampuni na hasa
makampuni ya kimataifa (Multinational Corporations). Nchi za Afrika
zimeathirika mno na mfumo wa kodi wa kimataifa na hivyo kupelekea fedha
nyingi kutoka Afrika kutoroshwa kwenda ughaibuni. Azimio la Tabora la
Chama cha ACT Wazalendo limeeleza kidogo kadhia hii ambayo Serikali za
Afrika hazitilii maanani kabisa licha ya taarifa nzuri ya Rais mstaafu
Thabo Mbeki wa Afrika ya Kusini.
Katika
kitabu cha 'Africa’s Odious Debts: How Foreign Loans & Capital
Flight Bled a Continet' waandishi Leonce Ndikumana na James Boyce,
wameonesha kwamba katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, jumla ya dola
za Kimarekani bilioni 11.4 (wastani wa shilingi trilioni 24)
zimetoroshwa kutoka Tanzania kwa njia mbalimbali.
Hizi
ni sawa na wastani wa dola za Kimarekani 285 milioni kutoroshwa kila
mwaka kuanzia mwaka 1970 mpaka 2010. Sehemu kubwa ya fedha hizi
zinatoroshwa na makampuni makubwa ya kigeni yanayofanya biashara na
kuwekeza hapa nchin. Africa Progress Panel na kikosi kazi kilichoongozwa
na Rais Thabo Mbeki ilieleza kuwa Afrika hupoteza zaidi ya dola za
kimarekani bilioni 50 kila mwaka kutokana na utoroshaji wa fedha
unaofanywa hususan na makampuni haya ya kimataifa.
Inasemekana
asilimia 30 ya utajiri wa fedha wa bara la Afrika umewekwa kwenye pepo
za kodi (tax havens) kwa mujibu wa kitabu cha 'The Hidden Wealth of
Nations' kilichoandikwa na Gabriel Zucman, mhadhiri wa London School of
Economics.
Katika
kitabu hicho, Zucman ameonyesha takwimu kutoka Benki ya Taifa ya Uswisi
zinazothibitisha kuwa takribani dola za kimarekani bilioni 150 kutoka
Afrika zimehifadhiwa kwenye mabenki ya nchi hiyo. Jumla ya Pato la Taifa
(GDP) ya nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki ni dola za kimarekani
147.3 bilioni, hivyo fedha za Afrika zilizopo Uswisi ni zaidi ya GDP ya
Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi kwa pamoja. Fedha hii ni
mara tano ya gharama za kujenga mradi wa Inga Dam kule Kongo ambao
ungeweza kuzalisha umeme wa kutosha bara zima la Afrika.
Pamoja
na mambo mengine, matundu haya ya ukwepaji kodi yamejengwa ndani ya
mfumo wa kodi za kimataifa. Kuna kitu kinaitwa kwa lugha ya kigeni Base
Erosion and Profit Shifting ikiwa na maana kuwa makampuni ya kimataifa
yanapowekeza hapa nchini huhamisha faida kupeleka nchi zenye viwango
vidogo vya kodi na hivyo kutolipa kabisa kodi hapa nchini ama kulipa
kodi kiduchu sana.
Kwa
mfano, katika kukokotoa kodi kampuni huondoa gharama za riba za mikopo,
bima na gharama za utawala na kinachobakia ndio faida ambayo hutozwa
kodi. Kampuni hizi huchukua huduma hizi za mikopo, bima na utawala
kutoka kwa makampuni dada na kuongeza gharama maradufu na hivyo
kuhamisha fedha hizi kana kwamba wanalipia hizi gharama na hivyo
kupunguza sana wigo wao wa kodi. Ndio maana siku za nyuma tulisikia
kampuni za madini hazilipi kodi ya mapato kwa sababu nyingi zilikuwa
zikitumia mtindo huu wa kumomonyoa wigo wa kodi.
Wakati
nikiwa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Madini ya Jaji Mark Bomani
tulikuta ushahidi wa kampuni ya Geita Gold Mines ambayo uwiano wa mtaji
wake na mikopo (debt-equity ratio) ulikuwa asilimia milioni 12. Hii
iliifanya kampuni hii kumomonyoa kila walichokipata katika uchimbaji wa
dhahabu nchini kwetu na kukihamishia njia kana kwamba ni malipo ya
mikopo waliyochukua kumbe ni mbinu ya kukwepa kodi na kupora dhahabu ya
Tanzania. Nilipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali, tuliagiza ukaguzi wa ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni ya
kimataifa na iligundulika kuwa karibia kila sekta ya uchumi ilihusika na
ukwepaji kodi.
Mfano
ambao huwa naukumbuka mara kwa mara ni mfano wa mauzo yetu ya Korosho
kwenda nje. Hupenda kuurudia na nitaurudia tena hapa. Mwaka 2011
Tanzania iliuza Korosho kwa nchi ya India. Kwenye rekodi ya Mamlaka ya
Mapato Tanzania ilionyesha kuwa tuliuza tani 80,000 za korosho kwa bei
ya dola za marekani 1000 kwa kila tani sawa na dola za kimarekani 80
milioni.
Uchunguzi
ulionyesha kuwa katika nchi ya India rekodi yao ya Korosho walizonunua
kutoka Tanzania ilikuwa ni dola za kimarekani 120 milioni kwa sababu wao
walinunua tani 120,000 za korosho kutoka Tanzania. Hii ina maana kuwa
tani 40,000 hazikurekodiwa kwenye forodha zetu na hivyo wauzaji kukwepa
kodi ya ushuru wa korosho wa zaidi ya dola za kimarekani 12 milioni.
Pia
kwenye kodi ya Mapato ya kampuni iliyouza korosho hizi mapato ya zaidi
ya dola 40 milioni hayatoonekana na hivyo kufanikiwa kukwepa kodi. Huu
ni mfano ninaopenda kuuleza katika kueleza namna mfumo wetu wa kodi
ulivyojaa matundu na kuhitaji kufanyiwa kazi kubwa ya kuufumua.
Kwa
hiyo makampuni yana njia nyingi za kukwepa kulipa kodi na hivyo
wamiliki wake kujilimbikizia mali nyingi na kuongeza tofauti ya kipato
miongoni mwa wananchi. Kama hatua madhubuti hazitachukuliwa tofauti ya
kipato itazidi kuongezeka na kuleta hatari kubwa kwa ustawi wa wananchi
na usalama wa nchi yetu.
Moja
ya suala ambalo chama cha ACT Wazalendo ililieleza na halikuelezwa na
chama kingine chochote katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015
ilikuwa ni hili la kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi ili kila
anayepaswa kulipa kodi alipe kwa haki na kwa uwazi.
Tuliahidi
"kuweka mfumo mpya wa kodi za kimataifa ili kuzuia makampuni ya
kimataifa kumomonyoa wigo wa kodi kwa kushiriki kikamilifu katika
kampeni za kimataifa za kurekebisha mfumo wa kodi za kimataifa, kupitia
mikataba ya kikodi na nchi nyengine ili kuzuia ukwepaji kodi na kujengea
uwezo kitengo cha kodi za kimataifa ili kudhibiti ukwepaji kodi".
Serikali ya Awamu ya Tano imefanya nini katika eneo hili?
Serikali
ya Awamu ya Tano ilisifika kwa makusanyo makubwa ya kodi katika miezi
yake ya mwanzo ya kuongoza nchi yetu. Lakini haijafanya juhudi yeyote ya
ndani au ya nje kuhakikisha kuwa nchi inaondoa tofauti kubwa ya kipato
kati ya wenye nacho na wasio nacho. Juhudi hizi za kukusanya kodi
hazijaweza kupunguza mzigo Wa kodi kwa wafanyakazi wa Tanzania.
Juhudi
za kuendesha kampeni ya kimataifa ili kuboresha mfumo wa kodi za
kimataifa zimeshuka chini na kiukweli kama nchi tumerudi nyuma wakati
dunia nzima inashiriki kwenye kampeni hizi. Juhudi za ndani za kuongeza
makusanyo ya kodi kama hazitatazama mfumo wa kodi za kimataifa, basi
hazitakuwa na faida yeyote na tutabakia na kodi za wafanyakazi na
vibarua tu tukiwakamua zaidi ili kupata fedha za kuendesha nchi yetu.
Tunapendekeza nini?
1.
Serikali ifanye marekebisho ya sheria mbalimbali za kodi zinazohusisha
makampuni ya kimataifa (MNCs) ili kuzuia kumomonyoa wigo wa kodi ( Base
Erosion and Profit Shifting) kunakofanywa na kampuni hizi. Hili
linawezekana kwa Serikali kuchukua hatua ya kupitia mikataba ya kikodi
(double taxation treaties) ambayo Tanzania iliingia na nchi nyingine
duniani.
Tafiti
mbalimbali katika eneo hili zinaonyesha kuwa Tanzania hupoteza 5% ya
Pato la Taifa kutokana na vitendo vya kampuni kubwa kukwepa kodi kwa
kutumia mbinu za kihasibu (tax planning measures). Serikali yetu
inapaswa kushirikiana na Serikali nyengine za nchi mbalimbali duniani
katika kampeni ya kimataifa ya haki za kodi (International Tax Justice
Movement).
Vyama
vya Wafanyakazi nchini vinapaswa kuwa mbele kuishinikiza Serikali
kushiriki kwenye kampeni hizi na pia kufanya mabadiliko makubwa kwenye
sheria zetu za kodi ili kulinda wigo wetu wa kodi.
2.
Serikali itazame upya michango ya wafanyakazi kwenye Mifuko ya Hifadhi
ya Jamii. Viwango vya michango Kwa Tanzania vipo juu mno na vinapunguza
kipato cha mfanyakazi na kuongeza gharama kwa waajiri. Michango ya
Hifadhi ya Jamii ishushwe mpaka jumla ya 12% ya mshahara; kwa Waajiri
kuchangia 7% na Wafanyakazi kuchangia 5% ya mishahara yao.
Hii
itasaidia kupunguza gharama za kuajiri kwa Waajiri. Vile vile Tozo ya
mafunzo SDL ishushwe mpaka 3% . Eneo hili ni muhimu liangaliwe kwa
muktadha wa kukuza ajira nchini hivyo ajira zinapoongezeka mapato kwenye
maeneo haya yanaongezeka pia.
3.
Serikali idhibiti mfumuko wa bei kuhakikisha inapunguza gharama za
maisha kwa wafanyakazi. Katika wakati kama huu ambao bei za vyakula
zimepanda zaidi ya mara 2 kipato cha wafanyakazi wengi nchini kimebaki
palepale, hali hii inaongeza ugumu wa maisha kwao. Ni muhimu Serikali
kuchukua hatua mahsusi kudhibiti mfumuko wa bei za vyakula nchini.
Mwisho,
Wafanyakazi wa Tanzania, nawakumbusha kuwa kuna mahusiano chanya kati
ya maslahi yenu na aina ya uongozi wa kisiasa uliopo kwenye nchi. Msikae
pembeni kwenye harakati za mabadiliko ya kisiasa nchini. Vyama vya
Wafanyakazi vina nguvu zaidi ya kuhamasisha na kuweka mazingira mazuri
ya kidemokrasia na utawala wa kikatiba nchini.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Dar Es salaam.
Mei 1, 2017
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni