Kutokana
na kauli hiyo, amemtaka Kitwanga ahame chama kama haoni jitihada za
kupeleka maji jimboni kwake zinazofanywa na Serikali.
Lwenge alitoa kauli hiyo bungeni juzi, alipokuwa akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018.
“Spika,
naomba nizungumzie mchango wa Kitwanga, ambaye alichangia hapa kwa
hisia kubwa akionyesha Serikali ya CCM haijafanya chochote kwenye Wilaya
ya Misungwi,” alisema na kuongeza:
“Nataka
nimuulize Kitwanga kama yupo hapa, kwamba hayo ni maneno yake au ni
maneno ya wananchi? Kama ni maneno ya wananchi, nitawaambia ni nini
kimefanyika Misungwi kwa sababu hata juzi tumesaini mikataba ya maji ya
shilingi bilioni 38 kutoka Ziwa Victoria kwenda Misungwi na Mwenyekiti
wa Halmashauri alikuwepo.
“Kitwanga
anaposema atakwenda kuhamasisha wananchi wakabomoe mtambo wa Iherere
maana yake analeta uasi au hathamini kazi iliyofanywa na chama chake?
“Kama
ni hivyo, sasa ajitoe kwenye chama kwa sababu Serikali imepeleka fedha
na kwa maendeleo yaliyofanyika, ni lazima tuwahamasishe wananchi kutunza
miundombinu iliyopo badala ya kwenda kuibomoa. Hata kwenye umeme huwa
tunaona wanaweka kwenye kijiji kimoja na kuruka hadi kijiji cha nne,
lakini hatujawahi kuona wanang’oa nguzo.”
“Kwa hiyo, nataka nimwambie kwamba, Serikali itaendelea kuboresha maji katika maeneo mbalimbali, ikiwamo Misungwi na Usagara.”
Lwenge
alisema kwa upande wa Usagara, Serikali itapeleka maji yanayosukumwa
kutoka Nyashishi, ambapo lita milioni tatu zitazalishwa na usanifu
unafanyika Buswelu.
“Sasa akisema haungi mkono bajeti maana yake hizi fedha tuzitoe tupeleke wilaya nyingine,” alisema.
Pamoja
na maelezo hayo, Lwenge alisema wizara yake kupitia Mamlaka ya Maji
Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza, imesaini mkataba wa Sh bilioni 38 kwa
ajili ya kupeleka maji Misungwi na kazi hiyo imefadhiliwa na Benki ya
Ulaya na Shirika la Maendeleo la Ufaransa.
Wakati huo huo, alisema Sh bilioni 3.5 zitatumika pia kupeleka maji katika vijiji mbalimbali vilivyopo wilayani Misungwi.
Majibu
hayo ya Lwenge aliyompa Kitwanga, ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi kabla uteuzi wake haujatenguliwa mwaka jana na Rais Dk.
John Magufuli, ni mwendelezo wa kauli zinazotolewa na wabunge wa CCM
baada ya kutoridhishwa na mchango wa mbunge mwenzao huyo.
Aliyeanza
kumshambulia Kitwanga ni Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma
(CCM), ambaye wiki hii alilitaka Jeshi la Polisi likampige mabomu
Kitwanga na wananchi watakaoandamana kwenda kung’oa mtambo wa maji.
“Jana
nilisikiliza mchango wa Kitwanga akilalamika kwamba atahamasisha
wananchi 10,000 wa Misungwi ili wakazime mashine ya maji Iherere,” alisema na kuongeza:
“Nilisikitika sana na nataka niwaulize kwamba, nyinyi mawaziri wa Magufuli hivi vile viapo mnavyokula mnajua maana yake?”
“Kama
hamjui maana ya hivi viapo, basi sina hakika kama mko sawasawa na kama
hamko sawaswa, Ndalichako (Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Mafunzo ya Ufundi), hebu pitisha operesheni ya vyeti feki huenda hapa
penyewe kuna feki za kutosha.”
“Hivi
inawezekana vipi mtu uliyekuwa waziri unasimama hapa na kusema
ulipokuwa waziri ulikuwa umebanwa kuzungumza na baada ya kufukuzwa sasa
uko huru kuzungumza?”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni