Jumatatu, 20 Juni 2016

WABUNGE WA UPINZANI WATOKA BUNGENI WAKIWA WAMEZIBA MIDOMO.




Wabunge wa Vyama vya Upinzani vinavyounda Ukawa, leo wametoka tena Bungeni kama walivyoazimia kukacha vikao vyote vinavyoongozwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, lakini wamekuwa na mtindo wa aina yake.

Tofauti na siku nyingine, leo wabunge hao wa upinzani wamejifunika midomo kwa plasta huku wakiwa wameandika jumbe mbalimbali za kuonesha kuminywa kwa haki ya kujieleza.

Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia aliwaambia waandishi wahabari nje ya ukumbi wa Bunge hilo kuwa wameamua kutoka nje ikiwa leo ni siku ya kuipigia kura bajeti ya Serikali kwani hawakushiriki kuijadili. Pia, alisema kuwa bajeti hiyo ni mbaya inayowaumiza wananchi.

“Ni fedha za watanzania wote walipa kodi tukiwemo sisi. Lakini democratic perspective inasema ‘hakuna kulipa kodi kama hakuna uwakilishi’. Sasa sisi tunawaambia Watanzania, tumejadili na bajeti hii ni mbaya… mbaya sana ya kuwaumiza Watanzania. Ni ya maumivu mabaya sana ya kuwaumiza Watanzania,” alisema Mbatia.

Alisema kwakuwa leo ni siku ya kupiga kura hawatashiriki kwa kuwa hawakushiriki kujadili bajeti hiyo bali wataenda kushtaki kwa wananchi.

Akizungumzia zuio la mikuano ya hadhara, Mbatia amesema kuwa mikutano hiyo itafanyika tu kwani haipangiwi na mtu mmoja bali ni kwa mujibu wa sheria na taratibu za kidemokrasia..




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni