BUNGE limepitisha kwa kauli moja
Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 2 ya mwaka 2016 ambayo pamoja
na mambo mengine, imeongeza adhabu kwa watu wanaowapa mimba au kuoa ama kuolewa
na mwanafunzi, sasa watafungwa jela miaka 30.
Sheria hiyo ilipitishwa jana bungeni
mjini Dodoma baada ya Muswada kuwasilishwa Juni 24, mwaka huu na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG) ambao baadhi ya wabunge walipata fursa ya kuuchangia.
Muswada huo ulilenga kufanya
marekebisho katika sheria 21 kwa lengo la kuondoa mapungufu yaliyobainika
wakati wa utekelezaji wa sheria hizo na umepitishwa kuwa sheria.
Sheria zilizopendekezwa kurekebishwa
na sheria hiyo ni pamoja na ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu;
Kudhibiti Usafirishaji Haramu wa Binadamu; Kanuni za Madai; Usajili wa
Makandarasi; Elimu; Ajira na Mahusiano Kazini na Sheria ya Taasisi za Kazi.
Muswada huo uliowasilishwa bungeni
na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju unatamka adhabu ya kifungo cha
miaka 30 jela katika marekebisho ya Sheria ya Elimu kwa watakaompa mimba,
kumuoa au kuolewa mwanafunzi.
Awali adhabu iliyotamkwa katika
sheria hiyo ya elimu ni mshitakiwa akibainika kuwa na kosa kutozwa faini ya Sh
500,000 na iwapo ni kosa la pili anatozwa faini ya Sh 500,000 au kifungo
kisichozidi miaka mitatu.
Akiizungumzia sheria hiyo
inayosubiriwa kusainiwa na Rais John Magufuli, Masaju alisema inawalinda watoto
wote chini ya miaka 18 walioko na wasio shuleni na kuwa kosa hilo likifanywa na
mtoto atahukumiwa kwa mujibu wa sheria ya mtoto.
Kifungu cha 60 A (i) kimeeleza kuwa
itakuwa kinyume cha sheria katika mazingira yoyote yale kwa mtu yeyote kumuoa
au kuolewa na mwanafunzi wa shule ya sekondari au ya msingi na atakayekiuka
atafungwa jela miaka 30.
Katika Sheria ya Taasisi za Kazi
inataka mwajiri anapokiuka masharti ya sheria ya kazi, ikiwa ni pamoja na
kuchelewesha michango ya waajiriwa, kutoza faini na Ofisa wa Kazi ya papo kwa
hapo isiyopungua Sh 100,000.
Wakichangia muswada huo, wabunge
wameonesha furaha yao juu ya Sheria ya Elimu inayohusu adhabu ya miaka 30 jela.
Hata hivyo, pamoja na furaha hiyo, baadhi ya wabunge wametoa angalizo la kutaka
kupimwa kwanza DNA kabla ya kutoa hukumu huku wengine wakitaka kuwapo kwa
nyongeza ya viboko.
Mbunge wa Geita Mjini, Constantine
Kanyasu (CCM) alipongeza marekebisho hayo na kutaka adhabu ya miaka 30 iongezwe
na kuchapwa viboko 12 kila mwezi mpaka aliyehukumiwa anamaliza kifungo kutokana
na wahalifu hao kuwa na mazoea ya kuzoea gereza.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Subira
Mgalu (CCM) alisema pamoja na serikali kuja na marekebisho hayo pia waangalie
namna ya kukabiliana na utoro shuleni ili kuwafanya wanafunzi kupata elimu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Njombe
Kusini, Edward Mwalongo (CCM) alitaka sheria imtake anayekutwa na kosa hilo
kuacha fedha za fidia ambazo mama atazitumia wakati mwanaume akiwa jela.
Akijibu hoja ya kutumika kwa vipimo
vya vinasaba (DNA), Masaju alisema kwa sasa utaratibu wa vipimo hivyo utatumika
mahakamani na waendesha mashitaka kuhakikisha hawaachi shaka kwenye ushahidi
kutokana na Tanzania kutokuwa na uwezo wa kumpima DNA mtoto akiwa tumboni.
Kuhusu Sheria ya Taasisi za Kazi,
Mbunge wa Viti Maalumu, Hawa Chakoma (CCM), alitaka adhabu hiyo kuongezwa ili
sheria kuleta tija na kutaka kazi ya kutoza faini hiyo isifanywe na Ofisa wa
Kazi kama ilivyotamkwa katika sheria badala yake ifanywe na Mamlaka ya
Usimamizi wa Mifuko ya Jamii (SSRA) kutokana na mifumo mizuri ya ufuatiliaji.
Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Sera,
Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama alisema serikali
imekuja na sheria hiyo ili kuwabana waajiri wanaochelewesha michango ya
waajiriwa na kuwa katika kutekeleza sheria waziri ataweka makundi na kuwa
kampuni zenye kipato kikubwa adhabu yao itakuwa kubwa zaidi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni