Jumatano, 29 Juni 2016

JESHI LA POLISI LAFANIKIWA KUKAMATA SILAHA 2 NA RISASI 23 NA KISU NA MAJAMBIA YALIYOTUMIKA KUUWA KIBATINI MKOANITANGA.



Jeshi la polisi mkowa wa Tanga limefanikiwa kukamata silaha mbili aina ya SMG na risasi 23, Bastola 1 risasi 1 Kisu na Majambia viliyotumika katika mauwaji yaliyofanyika mei 31 mwaka huu kata ya Kibatini Amboni mkoani Tanga.

Akizungumza waandishi wa habari ofisini kwake laeo, Kamanda wa polisi Mkoani Tanga, Leonard Poul, alisema kukamatwa kwa vifaa hivyo ni ushirikiano na vyombo vya usalama na wananchi.

Kamanda wa polisi mkoa Tanga Leonard Poul alisema walifanikiwa kuwakamata watu watatu walioshiriki kwenye mauwaji ya kikatili ya kibatini na kuwataja majina ya wahalifu kuawa ni Abdukalimu Singano, Sefu Jumanne na Ramadhani Muhamedi ambao wote walifariki baada ya kujaribu kukimbia eneo la msituni wa kibatini mara baada ya kuonyesha walipokuwa wamefukia silaha.

 
Kamanda Poul alisema kwa sasa mapango ya amboni ni salama na hayana tena matishio ya majambazi na kuwataka wananchi kuendelea na shughuli zao bila hofu yoyote.

 
Kamanda alisema “hawa ndiyo waliuwa watu 8  kwa kuchinjwa kikatili na matukio ya kuuwawa watu katika maduka makubwa na vituo vya mafuta na  uporaji, polisi walikuwa katika msako mkali na leo hii niseme Mapango ya Amboni ni Salama” alisema Poul.





Pia kamanda wa polisi mkoa wa Tanga amewataka wananchi na wakazi wa mkoa wa Tanga kutoa taarifa pindi wanapoona mtu wasiye mwelewa watoe taarifa kwa jeshi la polisi au kituo kilicho karibu nao.

Nahivi ni baadhi ya vyombo walivyokuwa wanatumia kwenye mapango ambavyo jeshi la polisi wameweza kuvishikilia. 


Jumatatu, 27 Juni 2016

SHERIA YA ADHABU KWA WATU WANAOWAPA MIMBA AU KUOA AMA KUOLEWA NA MWANAFUNZI NI MIAKA 30 JELA.



BUNGE limepitisha kwa kauli moja Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 2 ya mwaka 2016 ambayo pamoja na mambo mengine, imeongeza adhabu kwa watu wanaowapa mimba au kuoa ama kuolewa na mwanafunzi, sasa watafungwa jela miaka 30.

Sheria hiyo ilipitishwa jana bungeni mjini Dodoma baada ya Muswada kuwasilishwa Juni 24, mwaka huu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambao baadhi ya wabunge walipata fursa ya kuuchangia.

Muswada huo ulilenga kufanya marekebisho katika sheria 21 kwa lengo la kuondoa mapungufu yaliyobainika wakati wa utekelezaji wa sheria hizo na umepitishwa kuwa sheria.

Sheria zilizopendekezwa kurekebishwa na sheria hiyo ni pamoja na ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu; Kudhibiti Usafirishaji Haramu wa Binadamu; Kanuni za Madai; Usajili wa Makandarasi; Elimu; Ajira na Mahusiano Kazini na Sheria ya Taasisi za Kazi.

Muswada huo uliowasilishwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju unatamka adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela katika marekebisho ya Sheria ya Elimu kwa watakaompa mimba, kumuoa au kuolewa mwanafunzi.

Awali adhabu iliyotamkwa katika sheria hiyo ya elimu ni mshitakiwa akibainika kuwa na kosa kutozwa faini ya Sh 500,000 na iwapo ni kosa la pili anatozwa faini ya Sh 500,000 au kifungo kisichozidi miaka mitatu.

Akiizungumzia sheria hiyo inayosubiriwa kusainiwa na Rais John Magufuli, Masaju alisema inawalinda watoto wote chini ya miaka 18 walioko na wasio shuleni na kuwa kosa hilo likifanywa na mtoto atahukumiwa kwa mujibu wa sheria ya mtoto.

Kifungu cha 60 A (i) kimeeleza kuwa itakuwa kinyume cha sheria katika mazingira yoyote yale kwa mtu yeyote kumuoa au kuolewa na mwanafunzi wa shule ya sekondari au ya msingi na atakayekiuka atafungwa jela miaka 30.

Katika Sheria ya Taasisi za Kazi inataka mwajiri anapokiuka masharti ya sheria ya kazi, ikiwa ni pamoja na kuchelewesha michango ya waajiriwa, kutoza faini na Ofisa wa Kazi ya papo kwa hapo isiyopungua Sh 100,000.

Wakichangia muswada huo, wabunge wameonesha furaha yao juu ya Sheria ya Elimu inayohusu adhabu ya miaka 30 jela. Hata hivyo, pamoja na furaha hiyo, baadhi ya wabunge wametoa angalizo la kutaka kupimwa kwanza DNA kabla ya kutoa hukumu huku wengine wakitaka kuwapo kwa nyongeza ya viboko.

Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu (CCM) alipongeza marekebisho hayo na kutaka adhabu ya miaka 30 iongezwe na kuchapwa viboko 12 kila mwezi mpaka aliyehukumiwa anamaliza kifungo kutokana na wahalifu hao kuwa na mazoea ya kuzoea gereza.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Subira Mgalu (CCM) alisema pamoja na serikali kuja na marekebisho hayo pia waangalie namna ya kukabiliana na utoro shuleni ili kuwafanya wanafunzi kupata elimu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Njombe Kusini, Edward Mwalongo (CCM) alitaka sheria imtake anayekutwa na kosa hilo kuacha fedha za fidia ambazo mama atazitumia wakati mwanaume akiwa jela.

Akijibu hoja ya kutumika kwa vipimo vya vinasaba (DNA), Masaju alisema kwa sasa utaratibu wa vipimo hivyo utatumika mahakamani na waendesha mashitaka kuhakikisha hawaachi shaka kwenye ushahidi kutokana na Tanzania kutokuwa na uwezo wa kumpima DNA mtoto akiwa tumboni.

Kuhusu Sheria ya Taasisi za Kazi, Mbunge wa Viti Maalumu, Hawa Chakoma (CCM), alitaka adhabu hiyo kuongezwa ili sheria kuleta tija na kutaka kazi ya kutoza faini hiyo isifanywe na Ofisa wa Kazi kama ilivyotamkwa katika sheria badala yake ifanywe na Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Jamii (SSRA) kutokana na mifumo mizuri ya ufuatiliaji.

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama alisema serikali imekuja na sheria hiyo ili kuwabana waajiri wanaochelewesha michango ya waajiriwa na kuwa katika kutekeleza sheria waziri ataweka makundi na kuwa kampuni zenye kipato kikubwa adhabu yao itakuwa kubwa zaidi.

Ijumaa, 24 Juni 2016

MSWADA WA SHERIA YA MANUNUZI YA UMMA MWAKA 2016


WAZIRI WA UJENZI AKAGUA NA KUTOA MIEZI MIWILI KWA MKANDARASI WA KIWANJA CH



WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa miezi miwili kwa mkandarasi Chicco anaefanya upanuzi wa njia ya kuruka na kutua ndege katika uwanja wa ndege wa dodoma kuhakikisha kuwa ujenzi huo unakamilika.




 
Akizungumza mara baada ya kukagua kazi ya upanuzi wa uwanja huo, Prof. Mbarawa amemtaka Mkandarasi huyo kuhakikisha kuwa ujenzi wa uwanja huo unafanyika kwa kuzingatia viwango vilivyokubalika katika mkataba na kuukabidhi kwa wakati.
 

“Hakikisheni upanuzi huu unakamilika kwa wakati ili kuupa hadhi inayostahili uwanja wa ndege wa Dodoma, hasa mkizingatia umuhimu wake kitaifa’, amesema Prof. Mbarawa.

Naye Mkandarasi anaejenga uwanja huo amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa atahakikisha ujenzi wake unazingatia viwango na kuukabidhi katika muda uliokubalika kimkataba.

Zaidi ya shilingi bilioni 11.8  zinatarajiwa kutumia katika upanuzi huo na hivyo kuwezesha ndege nyingi zaidi kutumia uwanja huo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

WAFANYABIASHARA SOKO LA MGANDINI WALALAMIKIA UCHAFU WA SOKO HILO..



WAKATI wafanyakazi wa Idara ya Afya Jiji la Tanga wakikazana kuliweka Jiji  katika hali ya usafi imekuwa ni tofauti kwa soko la Mgandini.

Ni muda wa wiki mbili tu tangu wafanyakazi wa Idara ya Afya kufanya usafi katika soko hili la Mgandini ikiwa ni namna walivyo adhimisha siku ya mazingira duniani.

Kwa sasa hali ya Takataka katika soko hilo imerudi kama ilivyokuwa na kwasasa zimesogea hadi kwenye vizimba na kusababisha harufu kali na wadudu wa uchafu kuzagaa.

Akizungumza mmoja wa wafanyabiashara ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kufanya usafi mara moja sio kumaliza uchafu, hali ya soka inataka kufanyiwa usafi na kuzoa taka kila baada ya siku moja au mbili kwani ni sehemu yenye watu wengi.  

Halmashauri ya jiji la Tanga hufanya usafi katika mifereji na masoko kila siku lakini inadaiwa kuwa usafi katika masoko bado kutakuwa kunaongeza kasi kwa wafanyabiashara ili kutunza mazingira yao kuepuka miripuko ya magonjwa.

Jumanne, 21 Juni 2016

TANGA UWASA WAKABIDHI MADAWATI YENYE THAMANI YA MILION 3.



MAMLAKA ya Majisafi na usafi wa mazingira jiji la Tanga imekabidhi madawati 40 kwa ajili ya uchangiaji wa kampeni ya kutoa elimu bora kwa watoto wa shule za jiji la Tanga ili kutimiza agizo la Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuri.

Akizungumza wakati wa makabidhiano katika shule ya Jaje kata ya Tanga sisi Mkurugenzi  Mtendaji  Tanga Uwasa Eng. Joshua Mgeyekwa amesema madawati haya yenye thamani ya shilingi mil 3 ni sehemu ya kuwaunga mkono wateja wao wa Tanga Uwasa katika kuboresha mazingira ya kusomea watoto wao wanaosoma shule ya msingi jajae kuondokana na changemoto ya kukaa chini.

Pia Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga Uwasa amesema shule hii inayo changamoto ya mashimo ya choo na kuhaidi kutatua changamoto hiyo kuhakikisha walimu pamoja na wanafunzi wanafurahia mazingira yaliyopo shuleni.  
  
Eng. Mgeyekwa amesema mamlaka Majisafi na usafi wa mazingira iko tayari kuunga mkono shughuli zote zenye kuleta maendeleo katika Wilayani na Mkoani wa Tanga.

Akipokea madawati hayo Mkuu wa Wilaya ya Tanga Abdull Lutavi amewasii wanafunzi kuyatunza madawati hayo ili yaweze kutumika kwa vizazi hata vizazi.

Katika makabidhiano hayo ambayo yalifanyika katika shule ya Jaje Mkuu wa Wilaya alipokea madawati sabini arubaini kutoka Tanga Uwasa na mengine therathini kutoka kwa wadau wengine waliojitolea kuunga mkono agizo hili la Rais.





Naye Afisa Elimu Kata ya Duga Jani Lyatuu ameshukuru zoezi hili lililoanzwa na Mamlaka Majisafi na usafi wa mazingira  kwa shule ya msingi Jaje na kusema kwa sasa kata hii ya Duga  ina mapungufu ya madawati (628) kwa shule zote nne za kata hiyo na kuwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kama walivyofanya Tanga Uwasa.