Jumamosi, 29 Oktoba 2016

RAIS MAGUFULI ATOA UJUMBE KWA WATANZANI KATIKA SIKU YAKE YA KUZALIWA .



Rais wa jamuhuri ya Muungano Dkt John Pombe Joseph Magufuli Leo Oktoba 29 ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa ambapo alizaliwa Oktoba 29, 1959. 
 
Rais Magufuli alizaliwa mkoani Geita na kitaaluma yeye ni mwalimu aliyebobea katika somo la Chemistry.
 
Katika siku yake hii ya kuzaliwa, Rais Magufuli amewashukuru Watanzania wote kwa kuendelea kumuombea ambapo amesema kuwa ataendelea kufanyakazi kwa bidii na kuwatumikia watanzania wote kwa ajili ya maendelo ya nchi.

Ijumaa, 28 Oktoba 2016

MUUGUZI AFIKISHWA KIZIMBANI KWA UIZI WA MTOTO WA SIKU 4 ARUSHA.

MUUGUZI wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Scolastica Leoni (43) ambaye ni mkazi wa kata ya Sanawari amepandishwa kizimbani kujibu shitaka moja la kuiba mtoto mchanga wa kiume wa siku nne.

Akisomewa mashitaka na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Pennina Joackim mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Patricia Kisinda, ilidaiwa mshtakiwa alifanya kosa hilo Aprili 15, mwaka huu majira ya usiku wa manane akiwa kazini.

Mwendesha Mashitaka alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo akiwa kazini katika Hospitali ya Mount Meru wakati akifahamu wazi kufanya hivyo ni kosa kisheria na ni kinyume cha sheria na kanuni na taratibu za kazi. Alidai muuguzi huyo akiwa mtumishi wa umma katika hospitali hiyo aliiba mtoto muda mfupi baada ya kuzaliwa.

Alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha Kifungu 169 kifungu kidogo cha 1(a) cha Sheria na Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho 2002.
Mshtakiwa alikana shitaka na hakimu alisema dhamana ni haki ya mtu kwa mujibu wa sheria hivyo anatakiwa kudhaminiwa na wadhamini wawili wenye mali isiyohamishika yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 20.

TAARIFA YA IKULU: RAIS MAGUFULI AMEMTEUWA MKURUGENZI MTENDAJI WA SHIRIKA LA BIMA LA TAIFA (NIC)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  tarehe 27 Oktoba, 2016 amemteua Bw. Samwel Peter Kamanga kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC).

Bw. Samwel Peter Kamanga ameteuliwa kushika wadhifa huo kuanzia  tarehe 27 Oktoba, 2016.

Kabla ya uteuzi huo, Bw. Samwel Peter Kamanga alikuwa akikaimu nafasi hiyo.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam.

MABALOZI WA UMOJA WA ULAYA WATEMBELEA MKOANI TANGA




Mabalozi  wa umoja wa ulaya wakipokea taarifa ya mkoa katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Tanga.
 Mabalozi 12 wa umoja wa ulaya nchini Tanzania watembelea Bandari ya Tanga.



Mabalozi  wa umoja wa ulaya  nchini Tanzania Wakipokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa GPP Tanga






Mabalozi  wa umoja wa ulaya  nchini Tanzania watembelea Bandari ya Tanga na kufurahisha na utendaji kazi wa Bandari ya Tanga.
 

Wananchi wa chongoleani kijiji kilicho eneo litakalo jengwa bomba la mafuta wakibadilishana mawazo wakati wakisubiri ugeni wa Mabalozi wa umoja wa ulaya jijini Tanga. 


Alhamisi, 27 Oktoba 2016

MFANYABIASHARA MAARUFU ARUSHA KIZIMBANI KWA KUMNAJISI MTOTO WA KUMZAA.

Mfanyabiashara maarufu jijini Arusha na mkazi wa kata ya Sakina, Alistalius Silayo (45) amefikishwa mahakamani akituhumiwa kumnajisi mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miaka 11.

Akisomewa mashitaka na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Pennina Joackim ilidai kuwa mfanyabiashara huyo alitenda kosa hilo katika vipindi tofauti kati ya Januari na Septemba mwaka huu.

Mwendesha Mashitaka alidai mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Patricia Kisinda kuwa mshtakiwa alikuwa akifanya kosa hilo mara kwa mara katika miezi hiyo eneo la Sakina kwa Iddy yaliko makazi yake.

Alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha Kifungu cha 158 Kifungu kidogo cha 1(a) cha Sheria na Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 na kufanyiwa marekebisho 2002.

Baada ya kusomewa mashitaka, mshitakiwa alikana shitaka hilo na hakimu alisema dhamana iko wazi ya wadhamini wawili wanaotambulika kisheria. 
Mbali ya hilo, pia wadhamini hao lazima wawe na mali isiyohamishika yenye thamani ya zaidi Sh milioni 10 na wadhamini hawaruhusiwi kutoka nje ya Mkoa wa Arusha bila ya kibali cha Mahakama.

Hata hivyo, wadhamini hao walishindwa kukamilisha taratibu za dhamana mahakamani hapo na hakimu aliwapa muda kukamilisha taratibu katika saa za kazi na kuamuru mshtakiwa kurudishwa rumande hadi taratibu zitakapokamilika. 
Kesi hiyo itatajwa tena Novemba 10, mwaka huu kwani Mwanasheria wa Serikali alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Jumapili, 23 Oktoba 2016

UPUNGUFU WA MAJI KATIKA ZIWA RUKWA WAMSIKITISHA WAZIRI MAKAMBA ATOA MAAGIZO KWA WAKURUGENZI.



WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.January Makamba ameendelea na ziara ya kikazi katika Mkoa wa Rukwa. Katika ziara yake Waziri Makamba ameshuhudia uharibifumkubwa wa mazingira hususan pembezoni mwa ziwa Rukwa.

Waziri Makamba amewaambiwa wakazi wa Kijiji cha Nankanga kwamba mwaka 2000 kina cha maji katika ziwa Rukwa kilikuwa ni mita sita, na kwa mwaka 2016 chanzo hicho kimepungua hadi kufikia mita tatu.

“Tafiti zinaonyesha kuwa kupungua kwa kina hicho pamoja na mambo mengine kunasababishwa na kilimo cha milimani na kandokando ya ziwa, na ulishajiwa mifugo katika Vyanzo vya maji,” Makamba alibainisha.

Katika ziara yake baada ya kushuhudia uharibifu mkubwa kiasi hicho, Waziri Makamba ameazimia kulitangaza eneo la Ziwa Rukwa kama eneo mahsusi kwa mazingira na kanuni za matumizi ya maeneo hayo zitaandaliwa ilikunusuru Ziwa Rukwa.

Pia, wakurugenzi wote wa Halmashauri za Mkoa wa Rukwa wameagizwa kutenga pesa zitokanazo na tozo mbalimbali ili waweze kugharamia uwekaji wa alama maalumu ‘beacons’ ili kuainisha eneo tengefu na kuagiza kuwazoezi hili lifanyike haraka.

Aidha, Mhe. Makamba amesisitiza juu ya upandaji wa miti na ameonyesha masikitiko yake kwa Mkoa wa Rukwa kuwa na upungufu wa miti ya asili na ile ya kupanda kwa kiwango kikubwa. “nimetembea zaidi ya kilomita 200 sijaona miti iliyopandwa,” Makamba aliongezea.

Wakazi wa Mkoa wa Rukwa wamefahamishwa na kusisitizwa kuwa kuanzia mwakani itakuwa lazima kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuripoti na miti na kutakiwa kuitunza mpaka pale watakapomaliza shule. Waziri Makamba ameahidi kuleta wataalamu na kutoa orodha ya miche inayostawi katika kila kijiiji ili kurahisisha uoteshaji wa miti.

Katika hatua nyingine, Waziri Makamba amekutana na viongozi mbalimbali wa dini na wazee wa Mkoa wa Rukwa na kuwataka kuunda Kamati ya Amani,na kuahidi kugharamia Mkutano wa kwanza wa kuundwa kwa baraza hilo nakusisitiza agenda ya mazingira iwepo.

Mkoani Rukwa Waziri Makamba ametembelea mwalo wa ziwa Rukwa na kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo na Mkutano wa Hadhara.

Ijumaa, 21 Oktoba 2016

HESLB WAMETAKIWA KUONGEZA KASI YA UKUSANYAJI WA MADENI.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na waliohudhulia hafra ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa hosteli za wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam .

 
HABARI KAMILI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Magufuli ameagiza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kutumia Sheria zilizopo kuongeza kasi ya ukusanyaji wa madeni kwa wahitimu walionufaika na mikopo.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo jijini Dar es salaam wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa hosteli za wanachuo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam unajengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)  kwa gharama ya shilingi bilioni 10.

Amesema kuwa Serikali inadai takribani shilingi trilioni 2.6 kwa wahitimu walionufaika na mikopo ya Elimu ya juu.

“Serikali inawadai wahitimu walionufaika na mikopo ya Elimu ya juu takribani shilingi trillion 2.6 ambazo wanatakiwa kuzirudisha ili ziweze kutolewa kama mikopo kwa wanafunzi wapya na waliopo vyuoni” alifafanua Dkt Magufuli.

Aidha Dkt. Magufuli ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi kusimamia ipasavyo suala la utoaji wa mikopo kwa wanafunzi kwa kuzingatia vigezo vilivyopo kwani lengo la mikopo hiyo inawalenga watoto maskini.

Alisema kuwa kumekuwa na baadhi ya malalamiko ya kuwa  Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inafanya zoezi la ugawaji wa mikopo hiyo kwa upendeleo hivyo kuzitaka uongozi wa Wizara kushughulikia suala hilo.

Mbali na hayo Rais Magufuli amewataka wanufaika wa mikopo hiyo kutimia mikopo hilo kwa malengo mazuri katika kujinufaisha na masuala ya Elimu.

Naye Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Prof. Joyce Ndalichako  alisema kuwa mradi wa ujenzi wa hosteli hizo utasaidia kuwahudumia wanafunzi 3,840 ambapo unatarajiwa kuisha mwishoni mwa mwezi Desemba 2016.

Katika hatua hiyo Prof. Ndalichako alisema kuwa wanafunzi waliodahuiliwa kwa mwaka huu wapo 58,000 hivyo suala la wanafunzi 66,000 kukosa mikopo hiyo ni upotoshaji unaofanya na baadhi wa watu.

Mradi wa Ujenzi wa Hosteli za wanachuo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wenye majengo 20 kila jengo gorofa nne zenye vyumba 12 unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Desemba mwaka huu.