Jumatatu, 9 Januari 2017

ANGLICANA KWAFUKUTA CHIMELEDYA AMTIMUA ASKOFU MOKIWA, LAKINI KAGOMA KUTOKA .



MASHITAKA 10 yaliyofunguliwa na walei 32 wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam yakiwemo ya ufisadi wa mali za kanisa, yamesababisha Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dk Jacob Chimeledya kumvua uaskofu Mkuu wa Dayosisi ya Dar es Salaam Dk Valentine Mokiwa.

Hata hivyo Dk Mokiwa amegomea uamuzi huo kwa maelezokuwa mwajiri wake ni Sinodi ya Dar es Saalam ambayo ndiyo yenye uamuzi wa kumfuta kazi na sio askofu mkuu au askofu mwingine yeyote wa kanisa la Anglikana Tanzania.

Uamuzi wa kumvua uskofu ulichukuliwa juzi na Askofu Chimeledya baada ya Askofu Mokiwa kugoma kujiuzulu kama ilivyoshauriwa na nyumba ya maaskofu ambayo ilimkuta na hatia ya kufuja mali za kanisa hilo na kukiuka maadili ya kichungaji ambayo yalibainishwa kwenye ripoti ya uchunguzi iliyoundwa na kiongozi mkuu wa kanisa hilo nchini.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kanisa hilo zilieleza kuwa katika kikao kilichofanyika juzi kanisani Ilala, askofu Chimeledya na ujumbe wake walihudhuria kikao cha halmashauri ya kudumu ya dayosisi ya Dar es Salaam akatangaza uamuzi wa kumvua uaskofu Dk Mokiwa chini ya ulinzi wa polisi.

Licha ya uamuzi wa kumvua uaskofu, Dk Chimeledya pia aliagiza waraka unaoagiza askofu huyo kuondolewa madarakani, usambazwe kwenye makanisa yote yaliyoko chini ya dayosisi ya Dar es Salaam na usomwe jana kwenye ibada mbele ya waumini.

“Ni kweli kikao hicho kilifanyika jana, Dk Chimeledya alikuja na katibu mkuu na msajili wa kanisa kwenye kikao, lakini tulishangaa kwamba walikuja na askari polisi kinyume na utaratibu wa kanisa, alisoma maamuzi hayo aliyodai yametolewa na nyumba ya maaskofu,”alisema msemaji wa Dayosisi ya Dar es Salaam Yohana Sanga.

Dk Mokiwa agoma kung’oka
Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Dar es Salaam Padri Jonathan Senyagwa jana alisema habari hizo sio za kweli na barua ambazo zimesomwa katika baadhi ya makanisa jijini Dar es Salaam zilisomwa kwa makosa.

“Mwenye mamlaka ya kumfukuza kazi ni yule aliyemwajiri, na mwajiri wa Dk Mokiwa ni Sinodi ya Dar es Salaam...tutatoa tamko hivi karibuni kuthibitisha kwamba askofu wa jimbo bado hajafukuzwa,” alisema Padri Senyagwa.

Alisema waraka ambao umesambazwa na askofu mkuu wa Tanzania haujapitia kwenye halmashauri ya kudumu ya dayosisi ili kupata baraka zake na wala hauna baraka kutoka kwa sinodi ya dayosisi jambo ambalo linaufanya waraka huo ukose sifa za kutekelezeka.

“Ninachokwambia ni kwamba askofu wa dayosisi ya Dar es Salaam bado ni Mokiwa, hatuzitambui barua zilizosomwa katika baadhi ya makanisa,” alisisitiza katibu mkuu huyo wa Dayosisi.

Mgomo huo pia ulithibitishwa na Sanga, ambaye alifafanua kuwa juzi kulifanyika kikao kati ya viongozi wakuu wa kanisa na halmashauri ya kudumu ya dayosisi ya Dar es Salaam na kuelezwa na askofu mkuu wa Tanzania Dk Chimeledya hatua ya kumvua uaskofu Dk Mokiwa jambo ambalo halmashauri iligoma.

“Tulifanyia kikao chetu pale kanisa la Ilala, viongozi wetu wakuu walikuja na polisi wakatusomea huo waraka na kutangaza maamuzi hayo mbele ya halmashauri, lakini maamuzi hayo yaligomewa na wajumbe wa halmashauri ya Dayosisi ya Dar es Salaam,” alisema Sanga.

Alisema halmashauri iligoma kubariki uamuzi huo kwa sababu kanisa la Anglikana Tanzania lina kanuni na taratibu zake. 

Alifafanua kuwa waraka wa kumwondoa madarakani Dk Mokiwa lazima upate baraka za halmashauri ya kudumu ya dayosisi na sinodi ya dayosisi.

“Ule waraka tuliupitia na kubaini kuwa hauna baraza za nyumba ya maakofu, wala hauna baraka za halmashauri ya kudumu na Sinodi ya dayosisi ndio maana tuliwakatalia,” alisema Sanga na kuongeza kuwa maamuzi ya kumvua uaskofu Dk Mokiwa yamefanywa na askofu mkuu wa Tanzania, katibu mkuu na msajili wa kanisa na sio vikao vya kanisa.

“Ninachosisitiza hapa ni kwamba askofu wa dayosisi ya Dar es Salaam bado ni Dk Mokiwa, huo waraka uliotangazwa ni ushawishi wa watu wachache wanaotaka kumchafua kiongozi wetu wa Dayosisi,” alisema.

Aombwa ajiuzulu uaskofu 
Awali tume hiyo iliyoundwa kuchunguza tuhuma dhidi yake, baada ya kubaini makosa mengi yaliyofanywa na askofu huyo ilimshauri ajiuzulu wadhifa wake na awe tayari kufanya huduma nyingine ya kumtumikia Mungu.

“Hatua tunayoichukua ni kwa nia njema kabisa ya kulinusu kanisa letu ambalo limekuwa naheshima kubwa hapa nchini na duniani kote,” unasema waraka uliosaniwa na Dk Chimeledya.

Tume hiyo ilichukua uamuzi huo katika kutatua mgogoro uliopo ndani ya dayosisi ya Dar es Salaam:

“Nia yetu ni njema kabisa na hatuna chuki, uhasama wala upendeleo katika jambo hili, ifahamike kuwa vyombo vyote ndani ya kanisa ikiwemo nyumba ya maaskofu vinalifahamu jambo hili vyema, hivyo tulitarajia tutaungwa mkono ili kuisaidia dayosisi yetu ya Dar es Salaam kwenda mbele.”

Pia waraka huo unaeleza kuwa hiyo sio mara ya kwanza kanisa hilo kufanya maamuzi ya namna hiyo na kutoa mfano kuwa hata enzi za askofu Mokiwa akiwa askofu mkuu wa Tanzania alichukua hatua za kulinusuru kanisa lisipotee katika migogoro mbalimbali ikiwemo mgogoro wa dayosisi ya Tanga ambako alimtaka askofu wa dayosisi hiyo ajiuzulu kwa hiyari na alikubali.

Baada ya kutenguliwa uaskofu wa Mokiwa, Dayosisi ya Dar es Salaam itakuwa chini ya uangalizi wa uongozi wa askofu mkuu mpaka taratibu nyingine za kikanuni zitakapokamilika.

“Nina wasii Wakristo wote kwa nieaba ya Bwana Yesu Kristo tuendelee kuwa watulivu katika kuijenga dayosisi yetu na kanisa la Mungu kwa ujumla.”

Mashitaka 10 ya Mokiwa 
Askofu Mokiwa Machi 2015 alifunguliwa mashitaka 10 ambayo ni kuizuia dayosisi ya Dar es Salaam kupeleka michango pasipo maelekezo ya sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam, kuhamasisha dayosisi kujitoa katika udhamini wa kanisa Anglikana Tanzania (KAT) kwa lengo la kuifarakanisha dayosisi na jimbo kinyume na katiba ya dayosisi.

Mashitaka mengine ni kufuja mali za kanisa na kuingia mikataba kiholela yenye viashiria vya rushwa katika eneo la kanisa la mtoni Buza na miradi mingine, kushindwa kutatua migogoro inayohusu uwekezaji na maadili baina ya dayosisi na mitaa ya Magomeni ambao kuna mgogoro na Benki ya DCB, kanisa la Kurasini na mengine.

Askofu huyo pia anadaiwa kushindwa kutatua migogoro baina ya mapadiri na waumini na kutunza mali za kanisa katika mtaa wa Watakatifu wote Temeke na kutelekeza nyumba ya askofu iliyopo Oysterbay ambako imegeuzwa kuwa yadi ya kuuza magari.

Pia alilalamikiwa kushitakiwa mahakamani na Marehemu Christopher Mtikila na watu wengine watatu kwa kosa la kuwatishia silaha ya moto na kuwapapasa maungoni mwao bila ridhaa yao kinyume na maadili ya kikanisa.

Askofu Mokiwa pia analalamikiwa kuanzisha taasisi ya MEA Foundation iliyomwezesha kupokea fedha nyingi za wafadhili kwa ajili ya maendeleo ya dayosisi, lakini fedha zimefujwa na hesabu za chombo hazikuwahi kukaguliwa.

Tuhuma zingine ni kurejea kwa mchakato wa mapitio ya katiba mpya na kuvuruga mchakato wa awali wa maandalizi ya katiba mpya ya dayosisi kwa kutumia fedha za dayosisi na kutekelezwa askofu msaidizi dayososi ya Katanga Kalemi .

Alhamisi, 5 Januari 2017

Mambo yanayomleta waziri wa mambo ya nje wa China nchini Tanzania

 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China nchini
  Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. WANG Yi anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi nchini tarehe 09 Januari 2017. Mhe. Waziri Wang Yi atapokelewa na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga.
 
Madhumuni ya  ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri na ya kihistoria baina ya China na Tanzania ambayo yamedumu kwa zaidi ya miaka hamsini tangu kuanzishwa kwake pamoja ‎na kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano wa kiuchumi baina ya Tanzania na China.
 
Wakati wa ziara hiyo Mhe. Wang Yi atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa lengo la kumsalimia. 
 
Aidha, Mhe. Wang Yi atafanya mazungumzo rasmi na Mhe. Dkt. Mahiga kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Tanzania na China na ushirikiano wa kimataifa.
 
Itakumbukwa kwamba, Desemba 2015 kweneye Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na China, China iliichagua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi nne Barani Afrika zitakazowezeshwa kupiga hatua kwenye maendeleo ya viwanda. Kupitia mpango huo inatarajiwa viwanda takriban 200 vitajengwa au kuwekezwa nchini kutoka China kabla ya mwaka 2020.
 
Mpango huu unaenda sambamba na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2016/2020 na pia ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Joseph Magufuli wa kujenga Tanzania ya viwanda. Ni matarajio yetu kuwa, Watanzania takriban laki mbili watanufaika na ajira kupitia mpango huu mahsusi wa kuendeleza viwanda.
 
Mbali na mpango wa uendelezaji wa viwanda, viongozi hawa wawili watazungumzia miradi mingine ya miundombinu ambapo China imeahidi kuisadia Tanzania ikiwa ni pamoja na maboresho makubwa ya Reli ya TAZARA; Ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo pamoja na ujenzi wa Reli ya Kati.
 
Aidha, Mhe. Wang anatarajiwa kuzungumza na Mwenyeji wake kuhusu masuala ya ushirikiano wa kimataifa ikiwa ni pamoja na mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo China inaunga mkono msimamo wa Afrika na wa Tanzania wa kutaka Afrika ipewe viti viwili vya kudumu kwenye Baraza hilo na kura ya turufu. 
 
Vilevile viongozi hao watazungumzia masuala ya amani na usalama katika eneo la Afrika Mashariki pamoja na eneo la Bahari ya Kusini mwa China.
 
Mazungumzo hayo yatafuatiwa na Mkutano wa Mawaziri na Vyombo vya Habari (Joint Press Conference) ambapo wataeleza makubaliano waliyofikia kwenye mazungumzo yao.
 
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dar es Salaam
05 Januari, 2017

SHULE YA NAIBU WAZIRI WA JK,MAHIZA INAMADARASA MATATU PEKEE ,HUKU IKIWA NA MIKONDO SABA


SHULE  ya msingi iliyopewa jina la aliyekuwa naibu waziri  wa elimu wakati wa utawala wa Rais mstaafu Jakaya  Kikwete ,Mwantumu Mahiza mpaka  sasa inamadarasa matatu pekee hali inayosababisha wanafunzi wengine kusoma chini ya miti.

Shule iliyoko wilayani Mkinga mkoani Tanga inawanafunzi kuanzia darasa la kwanza hadi la saba  ambao hulazimika kusomea katika chumba kimoja kwa kupokezana na huku wengine wakipata elimu  chini ya miti. 

Hayo yamesababisha na Afisa Elimu msingi wilayani humo Zakayo Mrindoko wakati akiongea na Mtanzania kueleza changamoto za miundombinu ya kielimu inayoikabili   wilaya hiyo kwa sasa 

Alisema kuwa  shule hiyo ni miongoni mwa shule 11 zilizoanzishwa wakati wa mradi wa Mpango wa maendeleo ya Elimu ya msingi MMEM ambazo mpaka sasa zimeshindwa kuendelezwa kutoka na Halmashauri  kukosa fedha za kuendeleza majengo ya shule hizo pamoja na ofisi za walimu. 

Afisa Elimu huyo alisema kuwa uhaba huo wa vyumba vya madarasa wakati mwingine hulazimu wanafunzi wa madarasa mawili kusoma katika chumba kimoja jambo ambalo linaleta usumbufu  katika  utoaji wa elimu. 

Alisema kuwa ili miundombinu ya shule nyingi wilayani humo iweze kuwa vizuri na wanafunzi waweze kupata elimu katika mazingira bora kuna hitajika kiasi cha shilingi Bilioni mbili ambazo zitatumika kujenga madarasa 86..

"Kwa upande wa madawati hakuna shida ila tatizo kubwa lipo kwenye uhaba  wa madaraka, ofisi za walimu pamoja na watumishi kwa maana ya walimu ikama yao ni ndogo kwani tunaupungufu wa walimu 288 wa kada zote"alibainisha.

Hata hivyo Kaimu Mkurugenzi  wa Halmashauri  hiyo Michael Ndunguru alisema kuwa licha ya changamoto  za miundombinu zilizoko kwenye upande wa elimu wamefanikiwa kuvuka lengo la uandikishaji  wa wanafunzi wa darasa la kwanza kwa zaidi  ya 150%.

Alisema kuwa mwitikio huo umekuwa mkubwa kutoka na sera ya elimu bure inayotekelezwa kwa sasa nchini hivyo hata wazazi ambao kipato chao ni kidogo wameweza kuleta watoto wao. 

"Kwa hili la miundombinu  tumejipanga kuwaita wadau wa maendeleo  pamoja na wakazi wa wilaya hii waishio nje ya wilaya waweze kuchangia maendeleo  ya kielimu ili watoto wao waweze kupata elimu katika mazingira  bora badala  ya kusubiri serikali pekee"alisema Kaimu Mkurugenzi  huyo.

NIMR KUJENGA CHUO KIKUU CHA AFYA NA TIBA WILAYANI MUHEZA


TAASISI ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu NIMR inatarajia kuanzisha chuo kikuu cha afya na tiba ili kuweza kukabiliana na upungufu wa wataalamu wa utafiti wa magonjwa ya binadamu hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurungenzi wa Kituo cha utafiti cha Amani Dkt Willium Kisinza wakati akitoa taarifa ya kituo hicho kwa Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii,Wazee na Watoto Ummi Mwalimu wakati ya ziara yake katika kituo hicho.

Alisema kuwa chuo hicho kinatarajia kuanza udahili wa wanafunzi wake mapema mwakani kwa kushirikina na Chuo cha Kumbukumbu ya Sebastiani Kolowa kilichopo wilayani Lushoto.

Dkt Kisinza alisema kuwa kuanzishwa kwa chuo hicho kutaweza kusaidia kuongeza raslimali watu katika kuzalisha watafiti ambao wataweza kutumika kufanya  utafiti nchini na nje ya nchi .

“Tunawatafiti waliobeba katika ngazi za hadi  PHD hivyo tukaona ni wakati mwafaka  kuanzisha chuo ili  nguvu kazi iliyokuwepo tuweze kuitumia kufundisha wataalamu wengine Zaidi ambao watakuja kuwatumikia wananchi wa nchi hii”alisema Mkurungenzi huo.

Aidha Kwa upande wake Waziri Ummi Mwalimu alisema kuwa licha ya serikali kujitahidi kuzalisha wataalamu lakini bado hatujaweza kufikia kiwango kile kinachohitajika na umoja wa mataifaWHO.

Alisema kuwa kwa sasa serikali inajitahidi kujenga vyumba vya upasuaji katika kila wilaya hivyo ni vema chuo hicho kikaweza kuona umuhimu wa kuanzisha kozi ya maswala ya maabara pamoja na utafiti wa magonjwa ya binadamu.

“Tunanunua vifaa tiba vingi lakini changamoto kubwa iliyokuwepo ni uhaba wa wataalamu wa kutumia vifaa hivyo hususani sekta ya maabara na waatalamu wa dawa za usingizi hivyo kuanzishwa kwa chuo hicho kutasaidia kupunguza uhaba uliopo “alisisitiza Waziri Mwalimu.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Muheza Balozi Adadi Rajabu alisema kuwa wananchi wa Amani walikuwa wanaliona eneo hilo la ekari 227.8kama limetelekezwa huku likiwa na miundombinu ya kuanzishwa chuo.

Hivyo alisema  uanzishwaji wa chuo hicho utasaidia kusogeza huduma karibu na wananchi kwani eneo hilo litakuwa na hospitali kubwa ambao itaweza kuhudumia wananchi wengi

Jumanne, 3 Januari 2017

WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA CHINA WANG YI ATAFANYA ZIARA KATIKA NCHI TANO ZA AFRIKA



WAZIRI wa mambo ya nje wa China Wang Yi atafanya ziara katika nchi tano za Afrika zikiwemo Madagascar, Zambia, Tanzania, Jamhuri ya Kongo na Nigeria kuanzia tarehe 7 hadi 12 mwezi huu.

Hii ni desturi ya waziri wa mambo ya nje wa China kufanya ziara ya kwanza kila mwaka barani Afrika, ambayo imedumu kwa miaka 20.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Geng Shuang amesema mwaka huu ni mwaka wa kuendeleza kwa kina ushirikiano kati ya China na Afrika.

Ziara hiyo ya Wang Yi itahimiza makubliano mbalimbali yaliyofikiwa na rais Xi Jinping wa China na marais wa nchi za Afrika kwenye mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikano la China na Afrika uliofanyika mwaka jana mjini Johannesburg, Afrika Kusini.

WANAWAKE ZANZIBAR WAITAKA SERIKALI KUPUNGUZA ADA YA USAJIRI ARDHI.


SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imetakiwa kupunguza gharama za usajili wa ardhi kwa wanawake ili waweze kufikia na kumiliki ardhi na hivyo kuleta usawa wa kijinsia.

Amezungumza hayo Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) Zanzibar, Dk Mzuri Issa alisema wanawake wengi wamehamasika kujitokeza kupata hatimiliki lakini tatizo la urasimu na gharama kubwa za ada ni moja ya kikwazo kinachowakabili na kuwarudisha nyuma wanawake.

Kwa mfano alisema maombi 101 ya usajili wa ardhi yamefikishwa katika mamlaka mbalimbali ikiwemo kwa masheha katika hatua za awali pamoja na mamlaka ya ardhi katika hatua za mwisho lakini malalamiko makubwa yaliyojitokeza ni gharama kubwa.

“Tunashauri ni vizuri kwa serikali kupitia tena sera ya ardhi ili kuona mikataba ya kimataifa inavyolenga kutoa usawa wa kijinsia na kupunguza umasikini kwa jamii ya mwanamke,” alisema.

Alisema gharama za usajili zinazofikia sh 200,000 ni kubwa kuanzia kwa sheha hadi wilayani na katika Kamisheni ya Ardhi na watu wanaowasilisha maombi hayo kukwama katika hatua hizo.

Alisema pamoja na juhudi kubwa za kuimarisha ufikiwaji na umiliki wa ardhi kwa wananchi, rasilimali ya msingi ya maendeleo ni kiasi cha asilimia 20 tu cha wanawake ndiyo watakaofikiwa na huduma za umiliki wa ardhi.

Tamwa visiwani Zanzibar kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa kipo katika juhudi za kutoa elimu kwa wanawake kuona wanafaidika na fursa za kumiliki ardhi kwa maendeleo ya taifa na kiuchumi kwa ujumla.