Ijumaa, 16 Juni 2017

WAZIRI WA TAMISEMI AONYA WAKUU WA MIKOA, WILAYA WANAOWEKA WATU KIZUIZINI

Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene amewaonya wakuu wa mikoa na wilaya kutotumia vibaya madaraka yao ya kukamata watu walio kwenye himaya zao.

Ametoa onyo hilo leo (Ijumaa) alipojibu maswali ya wabunge waliotaka kufanyika marekebisho ya sheria inayowapa mamlaka wakuu hao ya kuwakamata na kuwaweka ndani wananchi wanaowatuhumu kwa lolote.

Licha ya kubainisha kwamba sheria hiyo haina tatizo, waziri amesisitiza: "Ukamataji unatakiwa ufanywe kwa mtu aliyetenda kosa la jinai au anayehatarisha usalama. Isiwe kwa show-off tu. Na mhusika anatakiwa kufikishwa mahakamani mara moja, asishikiliwe tu."

Amesisitiza kwamba wakuu hao ni wawakilishi wa Serikali kwenye maeneo yao, hivyo hawatakiwi kutumia vibaya madaraka waliyokasimiwa.

Katika siku za karibuni wakuu wa mikoa na wilaya wamekuwa wakilalamikiwa kuwaweka watu kizuizini pasipo kuwa na sababu za msingi, miongoni mwao wakiwamo waandishi wa habari.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni