Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amewaagiza Wakuu wa Mikoa kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa mpango wa
ujenzi wa viwanda katika maeneo yao ili kuwawezesha wananchi kuongeza
thamani ya mazao yao na kuzalisha ajira.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 13 Juni, 2017 Ikulu Jijini
Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Waakuu wa Mikoa ya
Tanzania Bara, kikao ambacho kimehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia
Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Mwanasheria
Mkuu wa Serikali Mhe. George Mcheche Masaju, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe.
Balozi John Kijazi na baadhi ya Mawaziri.
Mhe.
Rais Magufuli amesema kila Mkuu wa Mkoa anapaswa kufanyia kazi fursa za
uanzishaji wa viwanda katika eneo lake na kuhakikisha anashawishi
wawekezaji kuzitumia fursa hizo kama inavyofanyika katika Mkoa wa Pwani
ambako tangu Awamu ya Tano iingie madarakani viwanda vikubwa 83
vimejengwa na vingine kukamilika huku viwanda vidogo zaidi ya 120 pia
vikiwa vimejengwa.
Pamoja
na hilo Mhe. Rais Magufuli amewaagiza Wakuu wa Mikoa kuongeza juhudi za
utatuzi wa migogoro ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuharakisha mchakato wa
kuwanyang’anya hati za umiliki wa mashamba makubwa ambayo yanashikiliwa
na watu pasipo kuyaendeleza.
“Mashamba
yote yaliyotelekezwa, fuateni taratibu za sheria, yanyang’anyeni wapewe
Watanzania ambao wapo tayari kuyaendeleza, lakini fanyeni jambo hili
kwa kufuata utaratibu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amewatahadharisha Wakuu wa Mikoa hao dhidi ya watu
wanaofanya njama za kujimilikisha maeneo makubwa ya ardhi na kusababisha
wakulima na wafugaji kukosa maeneo ya kilimo na malisho na ametaka wote
watakaobainika kufanya njama hizo wafichuliwe na kunyang’anywa maeneo
hayo.
Mhe.
Dkt. Magufuli pia amewataka Wakuu wa Mikoa kushughulikia migogoro ya
wakulima na wafugaji na kuwahimiza wananchi kufanya kazi kwa juhudi na
maarifa na kuzalisha chakula cha kutosha katika maeneo yao.
Katika
kikao hicho Wakuu wa Mikoa wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi
zake za kuwapigania Watanzania hasa wanyonge na wamemuhakikishia kuwa
wataendelea kumuunga mkono katika juhudi hizo ikiwemo kudhibiti wizi wa
rasilimali za Taifa kama vile madini na maeneo ya hifadhi za
wanyamapori.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni