WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka maaafisa mifugo wote wa wilaya na mikoa
wabadilike ili sekta hiyo iweze kuongeza mchango wake kwenye pato la
Taifa.
“Katika
ziara zangu za mikoani nimekuwa nikionesha kutoridhishwa kwangu na
utendaji kazi wenu, na hasa jinsi tunavyoendesha ufugaji hapa nchini.
Mmeacha kazi ya kuwaongoza wafugaji, wanafanya wanavyotaka. Tunahitaji
kuona mabadiliko makubwa katika sekta hii,” alisema.
Alioa
agizo hilo jana mchana (Alhamisi, Juni 15, 2017) wakati akizungumza na
maafisa mifugo kutoka wilaya zote na mikoa yote wanaohudhuria kikao
alichokiitisha ili wajadili namna wanavyoweza kubadili uchungaji na
kufanya uwe ufugaji. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha
Mipango, nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Waziri
Mkuu alisema takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha Tanzania ni nchi ya tatu
barani Afrika na ya 11 duniani kwa ufugaji, ikiwa na ng’ombe takriban
milioni 24, nyuma ya Ethiopia yenye ng’ombe milioni 54 na Sudan yenye
ng’ombe 41.
“Wakati
sekta ya mifugo inatoa mchango usiozidi asilimia 10 kwenye Pato la
Taifa, wenzetu Ethiopia sekta hiyo hiyo inachangia asilimia 14 kwenye
pato lake na asilimia 16 ya fedha za kigeni. Nchi kama Botswana na
Namibia, nazo zinafanya vizuri kwenye sekta ya mifugo, pamoja na kwamba
wana mifugo michache, na eneo dogo la ardhi,” alisema.
“Ni
lazima tuanze kufikiri tofauti na kujitathmini kama kweli tunawatendea
haki Watanzania waliogharamia elimu yetu na wanaoendelea kutulipa
mishahara. Ningependa kupata ufahamu wenu wa kitaalam mna mipango gani
kuinua sekta hii kwa kuwafanya wafugaji wa Kitanzania wawe wafugaji
wanaotumia utaalam na hatimaye wao wenyewe na Taifa zima linufaike kwa
kupunguza umaskini,” alisisitiza.
Waziri Mkuu aliwataka maafisa hao wabadili mitazamo yao na waache kufanya kazi kwa mazoea. “Ni
lazima mtafute ufumbuzi wa kudumu kuhusu utatuzi wa migogoro baina ya
wakulima na wafugaji; na wafugaji na wahifadhi wa mapori tengefu au
mapori ya akiba.”
Amewataka
wajipange kuongeza uzalishaji wa mitambo na kuweka mazingira wezeshi
kwa sekta binafsi kuendelea kuzalisha mitamba ili kuhamasisha ufugaji wa
kisasa. Na pia watenge, wapime na kuwamilikisha wafugaji maeneo ya
ufugaji.
Alisema
ili kukuza sekta hiyo hawana budi kutoa elimu ya matumizi ya teknoljia
ya uhamilishaji, kuendeleza na kukuza masoko ya mifugo na mazao yake kwa
kujenga viwanda.
“Afisa
mifugo ni lazima ujue kwenye Halmashauri yako kuna minada mingapi na
inafanyika wapi. Kwenye bajeti hii, tumeondoa kodi ya makanyagio,
naamini hii itaongeza chachu ya wafugaji kupelekea mifugo yao minadani,” alisema.
Aliwataka
pia waendelee kuimarisha huduma za ugani katika ngazi za kata na vijiji
na kuhakikiasha wanaanzisha mashamba darasa ya mifugo.
“Jipangeni
kuanzisha mashamba darasa ya malisho katika kila Halmashauri. Kila eneo
mnaweza kuwa na shamba darasa kwa kuchagua mfugaji mmoja au wawili ili
wawe ndiyo mashamba darasa kwa wenzao,” alisema.
Mkutano
huo ambao umehudhuriwa na maafisa mifugo wa wilaya 185 na Maafisa
Tawala Wasaidizi wa Mikoa (wanaoshughulikia masuala la mifugo) zaidi ya
20, umehudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles
Tizeba, na Naibu Waziri wake, Bw. Willian Tate Ole Nasha, Makatibu Wakuu
wa Wizara za Kilimo na TAMISEMI, Wakuu wa Mapori ya Akiba, Wakurugenzi
wa Wizara ya Viwanda na Biashara na taasisi zinashughulika na maliasili;
na wakuu wa vyuo vya wanyamapori.
Mapema,
akimkaribisha Waziri Mkuu kuhutubia maafisa hao, Waziri wa Nchi (OR –
TAMISEMI), Bw. George Simbachawene alisema migogoro na chuki vinatokea
kwa sababu wahusika hawajaoanisha mifugo kama rasilmali na
kuzifungamanisha na uchumi wa watu wengine.
"Tuchukue
mfano, mtu akiwa na ng’ombe 1,000 katika eneo fulani. Kama uzalishaji
wake ukioanishwa na uchumi wa eneo husika, mafanikio lazima yatakuwa ni
ya eneo lile na siyo ya mtu binafsi,” alisema.