Jumanne, 25 Julai 2017

WAZIRI WA AFYA AWAPIGIA KIFUA WAGANGA WA TIBA ASILIA.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewataka waganga wakuu wa mikoa na wilaya kutowawekea vikwazo wataalamu wa tiba asili na mbadala ili waweze kujisajili na kutambulika kisheria.

Mwalimu ameyasama hayo jana  Jumatatu Julai 24 wakati akizindua Mpango Mkakati wa Tiba Asilia na Tiba Mbadala utakaoanza kutumika mwaka 2017 hadi mwaka 2022.

Alisema si lengo la Serikali kukandamiza au kuzuia tiba asilia bali inataka kuhakikisha dawa zinazotumika ni salama kwa afya za watumiaji.

“Ili kujua kama dawa ni salama lazima wajisajili, dawa zao ziangaliwe na inapothibitika kuwa ni salama basi zitumike, tusiwawakee vikwazo, ni wajibu wetu kuwawekea mazingira wezeshi kufikia hatua hiyo,” alisema.

Alisema zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wanatumia tiba mbadala na asilia hivyo ni muhimu kuwepo uangalizi wa kutosha kuhakikisha dawa hizo hazileti madhara kwenye jamii.

Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Dk Edmund Kayombo alisema watalaamu 16,200 pekee ndio wamesajiliwa kisheria kutoa tiba hizo.

“Tunawahamasisha waje kujisajili, wapo wanaojitokeza ila wengi wao wanakwepa kwasababu hawataki kuonyesha miti wanayotumia,”alisema.

MAANDALIZI YA UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI KATIKA BOMBA LA MAFUTA KUTOKA HOIMA UGANDA HADI TANGA TANZANIA.















Ijumaa, 16 Juni 2017

WAZIRI MKUU AKERWA NA UTENDAJI WA MAAFISA MIFUGO WA MIKOA NA WILAYA.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka maaafisa mifugo wote wa wilaya na mikoa wabadilike ili sekta hiyo iweze kuongeza mchango wake kwenye pato la Taifa.

“Katika ziara zangu za mikoani nimekuwa nikionesha kutoridhishwa kwangu na utendaji kazi wenu, na hasa jinsi tunavyoendesha ufugaji hapa nchini. Mmeacha kazi ya kuwaongoza wafugaji, wanafanya wanavyotaka. Tunahitaji kuona mabadiliko makubwa katika sekta hii,” alisema.

Alioa agizo hilo jana mchana (Alhamisi, Juni 15, 2017) wakati akizungumza na maafisa mifugo kutoka wilaya zote na mikoa yote wanaohudhuria kikao alichokiitisha ili wajadili namna wanavyoweza kubadili uchungaji na kufanya uwe ufugaji. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Mipango, nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Waziri Mkuu alisema takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha Tanzania ni nchi ya tatu barani Afrika na ya 11 duniani kwa ufugaji, ikiwa na ng’ombe takriban milioni 24, nyuma ya Ethiopia yenye ng’ombe milioni 54 na Sudan yenye ng’ombe 41.

“Wakati sekta ya mifugo inatoa mchango usiozidi asilimia 10 kwenye Pato la Taifa, wenzetu Ethiopia sekta hiyo hiyo inachangia asilimia 14 kwenye pato lake na asilimia 16 ya fedha za kigeni. Nchi kama Botswana na Namibia, nazo zinafanya vizuri kwenye sekta ya mifugo, pamoja na kwamba wana mifugo michache, na eneo dogo la ardhi,” alisema.

“Ni lazima tuanze kufikiri tofauti na kujitathmini kama kweli tunawatendea haki Watanzania waliogharamia elimu yetu na wanaoendelea kutulipa mishahara. Ningependa kupata ufahamu wenu wa kitaalam mna mipango gani kuinua sekta hii kwa kuwafanya wafugaji wa Kitanzania wawe wafugaji wanaotumia utaalam na hatimaye wao wenyewe na Taifa zima linufaike kwa kupunguza umaskini,” alisisitiza.

Waziri Mkuu aliwataka maafisa hao wabadili mitazamo yao na waache kufanya kazi kwa mazoea. “Ni lazima mtafute ufumbuzi wa kudumu kuhusu utatuzi wa migogoro baina ya wakulima na wafugaji; na wafugaji na wahifadhi wa mapori tengefu au mapori ya akiba.”

Amewataka wajipange kuongeza uzalishaji wa mitambo na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuendelea kuzalisha mitamba ili kuhamasisha ufugaji wa kisasa. Na pia watenge, wapime na kuwamilikisha wafugaji maeneo ya ufugaji.

Alisema ili kukuza sekta hiyo hawana budi kutoa elimu ya matumizi ya teknoljia ya uhamilishaji, kuendeleza na kukuza masoko ya mifugo na mazao yake kwa kujenga viwanda. 
“Afisa mifugo ni lazima ujue kwenye Halmashauri yako kuna minada mingapi na inafanyika wapi. Kwenye bajeti hii, tumeondoa kodi ya makanyagio, naamini hii itaongeza chachu ya wafugaji kupelekea mifugo yao minadani,” alisema.

Aliwataka pia waendelee kuimarisha huduma za ugani katika ngazi za kata na vijiji na kuhakikiasha wanaanzisha mashamba darasa ya mifugo. 
“Jipangeni kuanzisha mashamba darasa ya malisho katika kila Halmashauri. Kila eneo mnaweza kuwa na shamba darasa kwa kuchagua mfugaji mmoja au wawili ili wawe ndiyo mashamba darasa kwa wenzao,” alisema.

Mkutano huo ambao umehudhuriwa na maafisa mifugo wa wilaya 185 na Maafisa Tawala Wasaidizi wa Mikoa (wanaoshughulikia masuala la mifugo) zaidi ya 20, umehudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, na Naibu Waziri wake, Bw. Willian Tate Ole Nasha, Makatibu Wakuu wa Wizara za Kilimo na TAMISEMI, Wakuu wa Mapori ya Akiba, Wakurugenzi wa Wizara ya Viwanda na Biashara na taasisi zinashughulika na maliasili; na wakuu wa vyuo vya wanyamapori.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuhutubia maafisa hao, Waziri wa Nchi (OR – TAMISEMI), Bw. George Simbachawene alisema migogoro na chuki vinatokea kwa sababu wahusika hawajaoa​​nisha mifugo kama rasilmali na kuzifungamanisha na uchumi wa watu wengine.

"Tuchukue mfano, mtu akiwa na ng’ombe 1,000 katika eneo fulani. Kama uzalishaji wake ukioanishwa na uchumi wa eneo husika, mafanikio lazima yatakuwa ni ya eneo lile na siyo ya mtu binafsi,” alisema.

WAZIRI WA TAMISEMI AONYA WAKUU WA MIKOA, WILAYA WANAOWEKA WATU KIZUIZINI

Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene amewaonya wakuu wa mikoa na wilaya kutotumia vibaya madaraka yao ya kukamata watu walio kwenye himaya zao.

Ametoa onyo hilo leo (Ijumaa) alipojibu maswali ya wabunge waliotaka kufanyika marekebisho ya sheria inayowapa mamlaka wakuu hao ya kuwakamata na kuwaweka ndani wananchi wanaowatuhumu kwa lolote.

Licha ya kubainisha kwamba sheria hiyo haina tatizo, waziri amesisitiza: "Ukamataji unatakiwa ufanywe kwa mtu aliyetenda kosa la jinai au anayehatarisha usalama. Isiwe kwa show-off tu. Na mhusika anatakiwa kufikishwa mahakamani mara moja, asishikiliwe tu."

Amesisitiza kwamba wakuu hao ni wawakilishi wa Serikali kwenye maeneo yao, hivyo hawatakiwi kutumia vibaya madaraka waliyokasimiwa.

Katika siku za karibuni wakuu wa mikoa na wilaya wamekuwa wakilalamikiwa kuwaweka watu kizuizini pasipo kuwa na sababu za msingi, miongoni mwao wakiwamo waandishi wa habari.

Jumatano, 14 Juni 2017

RAIS MAGUFULI AKUTANA NA WAKUU WOTE WA MIKOA NCHINI NA KUTOA MAAGIZI MAZITO.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza Wakuu wa Mikoa kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa viwanda katika maeneo yao ili kuwawezesha wananchi kuongeza thamani ya mazao yao na kuzalisha ajira.

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 13 Juni, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Waakuu wa Mikoa ya Tanzania Bara, kikao ambacho kimehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Mcheche Masaju, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi na baadhi ya Mawaziri.

Mhe. Rais Magufuli amesema kila Mkuu wa Mkoa anapaswa kufanyia kazi fursa za uanzishaji wa viwanda katika eneo lake na kuhakikisha anashawishi wawekezaji kuzitumia fursa hizo kama inavyofanyika katika Mkoa wa Pwani ambako tangu Awamu ya Tano iingie madarakani viwanda vikubwa 83 vimejengwa na vingine kukamilika huku viwanda vidogo zaidi ya 120 pia vikiwa vimejengwa.

Pamoja na hilo Mhe. Rais Magufuli amewaagiza Wakuu wa Mikoa kuongeza juhudi za utatuzi wa migogoro ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuharakisha mchakato wa kuwanyang’anya hati za umiliki wa mashamba makubwa ambayo yanashikiliwa na watu pasipo kuyaendeleza.

“Mashamba yote yaliyotelekezwa, fuateni taratibu za sheria, yanyang’anyeni wapewe Watanzania ambao wapo tayari kuyaendeleza, lakini fanyeni jambo hili kwa kufuata utaratibu” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewatahadharisha Wakuu wa Mikoa hao dhidi ya watu wanaofanya njama za kujimilikisha maeneo makubwa ya ardhi na kusababisha wakulima na wafugaji kukosa maeneo ya kilimo na malisho na ametaka wote watakaobainika kufanya njama hizo wafichuliwe na kunyang’anywa maeneo hayo.

Mhe. Dkt. Magufuli pia amewataka Wakuu wa Mikoa kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji na kuwahimiza wananchi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na kuzalisha chakula cha kutosha katika maeneo yao.

Katika kikao hicho Wakuu wa Mikoa wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi zake za kuwapigania Watanzania hasa wanyonge na wamemuhakikishia kuwa wataendelea kumuunga mkono katika juhudi hizo ikiwemo kudhibiti wizi wa rasilimali za Taifa kama vile madini na maeneo ya hifadhi za wanyamapori.

Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

WASICHANA 700 WA MKOA WA TANGA WAMEKABIDHIWA VIFAA VYA UJASILIAMALI VYENYE DHAMANI YA SHILINGI MILIONI 153 KUTOKA SHIRIKA LA MAENDELEO LA BRAC.


Katibu Tawala mkoa wa Tanga Zena Said akiongea na wazazi na wasichana waliohitimu mafunzo mbalimbali vya ujasiliamali ambao wasichana 700 wamepatiwa vifaa vya ujasiliamali ili kuweza kujikimu kimaisha kutoka Brac Maendeleo Tanzania.
Meneja Mipango na Elimu Brac Tanzania Amina Shaaban akizungumza katika hafla ya kuwakabidhi vifaa vya ujasiliamali wasichana waliopata mafunzo mbalimbali  ya mkoani Tanga katika ofisi za Brac Makorola.
Walimu wa kozi mbalimbali zinazotolewa na Brac Maendeleo Tanzania.








Wanafunzi walio hitimu mafunzo ya ujasiliamali wakitoa maneno ya shukrani kwa viongozi wa  Brac Maendeleo Tanzania katika hafla fupi ya kukabidhiwa vitendea kazi . 
 Katibu tawala wa mkoa wa Tanga Zena Said pamoja na viongozi wa  Brac Maendeleo Tanzania wakikabidhi vifaa kwa wahitimu mafunzo ya ujasiliamali katika hafla fupi iliyo fanyika kwenye ofisi ya Brac Makorola Tanga ambapo wasichana 700 wamewezeshwa.





Wazazi wa wasichana waliomaliza mafunzo ya ujasiliamali yaliotolewa na Shirika la Maendeleo Brac Tanzania.
 


Wafanyakazi wa Brac Mendeleo Tanzania pamoja na viongozi wa mkoa wa Tanga wakiwa kwenye picha ya pamoja.