Jumanne, 6 Septemba 2016

SERIKALI YAKANUSHA TAARIFA INAYOSAMBAZWA KATIKA MITANDAO YA KIJAMII YA KUWA MAKAMU WA RAIS MAMA SAMIA SULUHU HASSAN AMEOMBA KUJIUZULU.


Ofisi ya Makamu wa Rais inakanusha taarifa inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, ameomba kujiuzulu nafasi yake na kwamba taarifa hiyo ni ya uzushi na uongo haina ukweli wowote.

Taarifa hiyo ni ya uchochezi inayolenga kuliweka Taifa kwenye taharuki.  Mhe. Makamu wa Rais yuko bega kwa bega na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kufanya kazi zao kwa mujibu wa Katiba ya nchi ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Ofisi ya Makamu wa Rais inawataka wananchi na Watanzania kwa ujumla kupuuza taarifa hiyo ambayo inalenga kupotosha umma kuhusu ushirikiano mzuri uliopo baina ya Viongozi wetu.

Mwisho, Ofisi ya Makamu wa Rais inawasihi Watanzania kufanya kazi kwa bidii na wajiepushe na vitendo vinavyolenga kuvuruga amani na utulivu nchini.
                                      

                                              Imetolewa na
                                        Ofisi ya Makamu wa Rais
                                                 Dar es Salaam

Jumatatu, 5 Septemba 2016

WIZARA YA ELIMU TEKNOLOJIA NA MAFUNZO YA UFUNDI YAWATAKA VIJANA KUJIAJIRI KWA ELIMU WALIYOPATA.



SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imewaasa vijana waliomaliza shule kuacha kujibetweka bali watumie elimu waliyoipata kujitafutia ajira ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.

Kauli hiyo imetolewa jana Jijini Dar es Salaam na Kaimu Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Nicholaus Bureta wakati wa ufunguzi wa mkutano wa vijana wa Afrika unaojadili changamoto zinazowakabili vijana katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Bureta alisema kuwa Serikali  inatoa elimu bora ili kuhakikisha vijana wanapata uwezo na maarifa yatakayowasaidia kujiajiri hata wasipopata nafasi za kuajiriwa katika taasisi na ofisi za umma pamoja na kuitumia elimu hiyo katika kupambana na vitendo vya rushwa.

“Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inatutaka tuwe na watanzania walioelimika na wenye mtazamo chanya ambao utahakikisha jamii yetu inabadilika kufikia uchumi wa kati hivyo vijana msikae kusubiri ajira bali mjifunze jinsi ya kujiajiri kutokana na elimu mliyoipata mashuleni”, alisema Bureta.

Kwa upande wake Afisa Habari wa Umoja wa Mataifa (UN), Stellah Vuzo aliwapongeza vijana hao kuamua kukusanyika kuchangia mawazo yao juu ya matatizo yanayowakabili kwani vijana wana nafasi kubwa ya kuhakikisha malengo mbalimbali yanatekelezeka.

Aidha, aliongeza kuwa Umoja wa Mataifa umemteua balozi kijana ambaye anashughulikia ajira za vijana hivyo aliwaomba vijana walioshiriki katika mkutano huo kuyafikisha mawazo hayo kwa balozi huyo ili yaweze kupatiwa ufumbuzi.

Naye Mkuu wa Utafiti kutoka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (PCCB), Daniel Pundu alisema kuwa tatizo la rushwa haliwezi kuisha endapo vijana hawatashirikishwa hivyo amewasisitiza vijana kushirikiana na Serikali kuchukua hatua za kupambana na rushwa ili kuhakikisha rushwa inaondoka.

“Tunajua kuwa vijana ndio nguvu kazi ya Taifa na ndio sababu tunawasisitiza kupambana na rushwa, kwa kulitambua hilo Serikali imeanzisha vilabu vya wapinga rushwa katika shule za sekondari na vyuo vikuu vikiwa na lengo la kuhakikisha vijana wanahusika kwenye mapambano hayo”, alisema Pundu.